VIDEO: Madaktari, wauguzi Marekani walilia vifaa vya kujikinga virusi vya corona

Muktasari:

  • Jiji la New York limeshambuliwa vibaya na ugonjwa wa virusi vya corona huku zaidi ya watu 50,000 wakiwa na maambukizi na 6,500 kati yao wakiwa wamelazwa hospitalini.

Wafanyakazi wa afya katika jiji la New York lililoshambuliwa vikali na virusi vya corona, wanafanya kazi kwa muda mrefu huku wakiwa na mahitaji makubwa ya vifaa vya kujikinga-- na wakati maambukizi yakizidi, ongezeko la hofu ya usalama wao ni kubwa.
Wakati wakitoa kilio hicho, wakazi wa jiji hilo walikuwa wakishangilia kazi ya madaktari na wauguzi ambao wamekuwa wakiwajibika kuokoa maisha ya watu licha ya upungufu wa vifaa.
Kelele za makofi na sauti za kushangilia zilisikika kutoka katika majengo marefu ya Manhattan ambako kuna amri ya watu kutotoka majumbani kuwaepusha na maambukizi ya virusi hivyo ambavyo vimeambukizi zaidi ya watu 50,000, huku 6,500 kati yao wakiwa wamelazwa hospitalini.
Madaktari na wauguzi wanafanya kazi usiku na mchana kuhudumia wagonjwa waliokumbwa na maambukizi yanayoenea kwa kasi, wakiweka hatarini maisha yao katika kipindi hiki ambacho ugonjwa wa homa kali ya mapafu, Covid-19, unaisumbua dunia.
Katika wiki hiyohiyo, Marekani imegeuka kuwa taifa linaloongoza kwa ugonjwa huo wa dunia-- ikiwa na watu 120,000 waliothibitika kupata maambukizi na wengine 2,000 waliofariki.
Kifo cha mtu mwenye umri wa miaka 48 kiliibua hofu kwa wafanyakazi wengi wa afya ambao wamelalamikia upungufu wa vifaa, kama magauni ya plastiki ya kujikinga na barakoa (mask) maalum kwa ajili ya hospitali.
"Ni ujuha," alisema Andrew, daktari wa magonjwa ya akili katika hospitali moja ya New York ambaye aliomba jina lake lisitajwe na hivyo kubadilishwa.
Hivi sasa amewekwa chini ya karantini nyumbani akihofiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.
"Hakuna fedha za kutosha, hakuna upimaji wa kutosha, hakuna vifaa vya kutosha vya kujikinga kwa watu wanaoshughulikia hili -- si madaktari pekee, lakini wauguzi na wafanyakazi wengine -- kila mmoja hospitalini ambaye yuko katika hatari kubwa ya virusi," alisema katika mahojiano na AFP huku akikohoa.
Karibu Wafanyakazi 20 wa afya waliandamana kupinga mazingirayao ya kufanyia kazi Jumamosi asubuhi nje ya Kituo cha Afya cha Jacobi mjini Bronx.
"Tunaweka hatarini maisha yetu kuwaokoa," liliandikwa moja ya mabao yao, likiomba "#PPENow" -- barakoa, glovu na vifaa vingine vya kujikinga.
Diana Torres, aliyesoma na Kelly katika chuo hicho cha kundi la hospitali za Mount Sinai, walisema wafanyakazi wa afya wamechukizwa kwamba mwenzao amepoteza maisha kwa sababu ya matatizo hayo.
Diana, ambaye ana watoto watatu, aliiambia AFP kuwa kuna sehemu katika hospitali ambazo zimefurika wagonjwa wa virusi vya corona.
Anafanya kazi idara ya ushauri na binafsi ameshashughulikia angalau wagonjw watatu walioambukizwa virusi hivyo -- labda wengi zaidi kwa kuwa hakuna upimaji wa kutosha wa kuwa na uhakika.
Kifo cha Kelly kuliibua hasira katika mitandao ya kijamii kuhusu ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kujikinga.