Madaktari Zimbambwe wapuuza amri ya mahakama, waendelea kugoma

Muktasari:

Madaktari hao wanaoendelea na mgumu kwa wiki sita sasa walisema hawawezi kurejea kazini kwa sababu ongezeko waliloahidiwa na Serikali bado lipo chini.

Harare, Zimbambwe, Madaktari nchini Zimbabwe wamepuuza amri ya mahakama iliyowataka kurudi kazini na kudai kuwa wataendelea na mgomo.

Madaktari hao walisema hawawezi kurejea kazini kwa sababu ongezeko waliloahidiwa na Serikali bado lipo chini.

Mwishoni mwa wiki Serikali nchini humo iliahidi ongezeko la mshahara kwa wahudumu hao wa sekta ya afya na kuwataka kurejea kazini kama kawaida baada ya kuendesha mgomo wa zaidi ya wiki sita wakishinikiza kuongezewa maslahi yao.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, kwa sasa madaktari hao wanalipwa mshahara wa dola 100 karibu Sh250,000.

Ijumaa iliyopita Mahakama mjini Harare nchini humo ilitoa hukumu yake kuwa mgomo huo haukuwa halali na kuwapa saa 48 kuanza tena majukumu yao.

Hata hivyo, wakizungumza na waandishi wa habari viongozi wa Jumuiya ya Madaktari wa Hospitali Zimbabwe (ZHDA) walisema hawawezi kufuata agizo la mahakama kwa sababu wanakosa njia ya kupata kazi au kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.

Jumuiya hiyo pia ilisema wanakamilisha taratibu za kukata rufaa katika Mahakama Kuu ili kuhakikisha haki yao inapatikana.