Maelfu Iran yaomboleza kifo cha Qassem Soleimani

Muktasari:

  • Mwili wake uliwasili kutoka Baghdad, Iraq alikouawa na utazikwa kesho katika mji aliozaliwa katikati ya Iran

Ahvaz. Maelfu ya raia wa Iran wamefurika katika miji ya Ahvaz na Mashhad nchini humo leo, kuomboleza kifo cha jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran Qassem Soleimani, alieuawa katika shambulio la Marekani mjini Baghdad nchini Iraq.

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei ameongoza swala mbele ya majeneza na watu waliouawa akiwamo Someimani ambaye mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho Jumanne kijijini kwake katikati ya Irani.

Mauaji hayo yaliamrishwa na Rais Donald Trump, ambaye amesema kamanda huyo wa kikosi cha Qudus cha jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi la Iran, alikuwa anapanga mashambulizi dhidi ya wanadiplomasia na wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.

Khamenei amepa kulipiza kisasi na kutangaza siku tatu za maombolezi, lakini Trump ameionya Iran na kusema Marekani itayalenga maeneo 52 ambayo ni muhimu kwa Iran, na kwamba itawashambulia haraka na kwa namna ambayo hawajawahi kushuhudia.