Mafuriko yakwamisha safari za treni Nairobi

Nairobi. Maelfu ya wakazi wa jiji la Nairobi leo wamelazimika kutembea umbali mrefu na wengine kutumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri, baada ya treni zinazotoa huduma jijini humo kusitisha kutokana na maeneo mengi ya reli kujaa maji.

Abiria wengi walifurika kwenye vituo mbalimbali vya treni, lakini baada ya kusubiri kwa muda na kupokea habari kuwa huduma hizo hazitakuwapo, walilazimika kutembea kwa miguu.

Baadhi yao pia walilazimika kulipa nauli ya juu ya magari yaliyotumia fursa ya kukosekana kwa treni kuongeza nauli wanazotoza.

Kwa mfano, magari yanayohudumia barabara ya Embakasi, ambayo kwa kawaida hulipisha nauli ya kati ya Sh40 na Sh50, yaliripotiwa kupandisha hadi Sh100 yalipofahamu hakuna treni.

Kulikuwa na uhaba wa magari katika maeneo mengi yanayohudumiwa na treni, huku vituo vingi vya magari vikionekana kujaa watu.

Kila siku, mji wa Nairobi unahudumiwa na treni nane zinazobeba maelfu ya watu.

Katika taarifa kwenye mitandao yake ya kijamii, kampuni ya Kenya Reli nchini Kenya ambayo hutoa huduma hizo kwa maelfu ya wakazi wa Nairobi, imethibitisha kusimamishwa kwa safari za treni jijini humo.

“Kutokana na mafuriko katika maeneo kadhaa ya reli za treni jijini Nairobi, hatuna uwezo wa kutoa huduma kutoka makao makuu ya treni za Nairobi kati ya kituo kikuu na vituo vya Kikuyu, Ruiru, Embakasi na Syokimau kwa sababu za kiusalama.”

“Tunaomba wateja kutafuta njia mbadala kufika wanakoelekea. Tunashughulika kurejesha huduma hizi kwa haraka iwezekanavyo. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote ambao umetokana na hali hii,” taarifa hiyo imesema.