Makaburi 4,163 ya pamoja yagundulika Burundi

Muktasari:

 Ni kufuatia uchunguzi wa mwaka mmoja ambako majina ya watu 142,505 waliouawa tangu mwaka 1962 ya uhuru yalitambulika.

Gitega, Burundi. Makaburi  4,163 ya pamoja yamepatikana katika miji miwili tofauti nchini Burundi.

Makaburi hayo yalipatikana kufuatia uchunguzi uliofanywa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa Tume ya Maridhiano nchini Burundi iliyopewa jukumu la kubaini ukweli katika nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo wa kikabila tangu ilipopata uhuru, imebaini pia majina ya watu 142,505 waliouawa tangu mwaka 1962 ya uhuru.

Vilevile, Tume hiyo ilisema kuwa makaburi hayo yaligundulika katika mikoa 18 ya nchi hiyo.

“Makaburi 640 yalipatikana katika eneo la Gitega ambalo ni makao makuu mapya ya Serikali,” inasema ripoti hiyo ilitolewa jana Jumanne Januari 14.

Siku ya Jumatatu Tume hiyo iliweka wazi kwa umma kaburi la pamoja lililopatika katika jiji la Bujumbura ambako mabaki ya miili ya watu kati ya 250 na 270 ilipatikana.

Tume hiyo ilisema watu hao wanasadikiwa kuuawa wakati wa makabiliano kati ya majeshi ya jamii ya Watutsi na Wahutu baada ya kifo cha Rais Melchior Ndadaye mwaka 1993.

"Makaburi mengi zaidi yanatarajiwa kupatikana kwa sababu watu wanayajua lakini wanaogopa kuzungumza,” alisema Pierre-Claver Ndayicariye, mwenyekiti wa Tume hiyo alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo kwa bunge jana Jumanne.

Baada ya kuonyesha makaburi ya pamoja ya Bujumbura, Naibu mwenyekiti wa Tume hiyo Noah Clément Ninziza aliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kwamba “baadhi ya watu wamewatambua jamaa zao katika mabaki hayo.

Baada ya kupata uhuru mwaka 1962 Burundi ilikabiliwa na mzozo wa kikabila kati ya Wahutu na Watutsi uliochochewa kisiasa na kusababisha mauaji ya mamia ya watu katika miaka ya 1965, 1969, 1972, 1988 na 1993.

Ndayicariye alisema kupata ukweli kuhusu kile kilichofanyika kutasidia kuleta maridhiano kati ya waliotekeleza na waathiriwa wa mauaji hayo ili kufikia amani ya kudumu nchini humo kwa vizazi vijavyo.