Mamia wamiminika mazishi ya Qasem Soleimani

Muktasari:

Aliuawa na kombora la Marekani mjini wa Baghdad, Iraq Ijumaa iliyopita

Idadi kubwa ya waombolezaji waliyovalia mavazi meusi wamejitokeza kutoa heshima za mwisho kwa kamanda wa jeshi la Iran Qasem Soleimani kabla ya mazishi yake katika mji alikozaliwa, Kerman, leo Jumanne.

Soleimani aliuawa katika mapambano ya anga na jeshi la Marekani nchini Iraq Ijumaa iliyopita baada ya Rais Donald Trump kutoa amri auawe.

Mwili wake sasa upo katika mji wa Kerman aliokuwa akiishi, kusini mashariki mwa Iran.

Kundi kubwa la watu wamejitokeza katika shughuli hizo za mazishi mjini Tehran.

Iran imeapa kulipiza kisasi cha mauaji ya kiongozi huyo wa jeshi la Iran, huku Marekani nayo ikibainisha maeneo 53 yakiwamo ya kihistoria itakayoyashambuliwa ikiwa maslahi yake yataguswa.

Soleimani (62), alikuwa akiongoza kundi la jeshi la Quds ambalo kazi yake kubwa ni kulinda usalama wa Iran na kuongeza ushawishi wa taifa hilo la Mashariki ya kati.

Katika mji wake, Soleimani alitambuliwa kama shujaa wa taifa na alifahamika kama mtu wa pili ambaye ana nguvu zaidi katika taifa hilo, baada ya kiongozi wa Iran Khamenei.