Maporomoko ya tope yaua 39 Kenya

Sunday November 24 2019

 

Maporomoko ya udongo na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo la Pokot magharibi mwa Kenya, yameua watu 39, maofisa wamethibitisha.

Maporomoko hayo yameathiri zaidi vijiji vya Nyarkulian na Parua, ambako nyumba za wakazi zilibomolewa na maji ambayo pia yalilisomba daraja, kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizoathiriwa na mkasa huo.

''Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya mkasa huu, kwa wale waliojeruhiwa na ambao wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali, nawaombea uponyaji wa haraka,'' alisema Rais Kenyatta, huku akiagiza vikosi vya jeshi kuhusika katika uokoaji.

Rais aliagiza ndege ya kijeshi kupelekwa katika eneo hilo kusaidia katika shughuli ya uokoaji na kutoa wito kwa mamlaka katika eneo hilo kushirikiana na asasi za usalama kufanikisha operesheni hiyo.

Chifu Joel Bulal wa eneo la Nyarkulia, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema shughuli za uokoaji zinaendelea kuwatafuta wale ambao hawajulikani waliko.

Advertisement

Kamishna wa jimbo hilo, Apollo Okelo amesema watu wengine wengi huenda wamekwama chini ya matope na kuwa shughuli ya kuwaokoa zinaathiriwa na hali mbaya ya hewa.

"Tunajaribu kutafuta mahali ambapo daraja limesombwa na maji ya mafuriko," alinukuliwa na mtando wa habari wa Standard nchini Kenya.

Shughuli za uchukuzi zimeathirika kabisa katika eneo hilo huku magari zaidi ya 200 yakikwama.

Picha zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha miti iliyosombwa na maji na mingine kung'olewa, huku matope yakisambaa barabarani.

Shirika la Msalaba mwekundu limethibitisha ripoti zinazoashiria tukio la maporomoko makubwa ya matope.

Mvua kubwa zimetikisa katika eneo la Afrika Mashariki na pembe ya Afrika kwa wiki kadhaa sasa.

Mbali na Kenya, kijiji kizima kimeripotiwa kusombwa na maji nchini Sudan Kusini huku visa ajali ya maporomoko ya ardhi ikiripotiwa wilayani Sengerema, Tanzania, Ethiopia na Somalia.

Wanasayansi wanasema hali mbaya ya hewa inatarajiwa kukumba baadhi ya nchi katika kanda hiyo kwa sababu viwango vya joto katika Bahari ya Hindi vikitarajiwa kupanda kupita kiasi cha kawaida, hali ambayo huenda ikasababisha mvua kubwa.

Advertisement