Marais wengine wa Marekani akiwamo Clinton waliwahi kushitakiwa

Andrew Johnson (kushoto) na Bill Clinton (kulia) walikutwa na hatia, lakini waliokolewa na Bunge la Seneti. Nixon (katikati) alijiuzulu mwenyewe.

Washington. Licha ya Rais wa 45 wa Marekani Donald Trump kukabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka kiasi cha kuandaliwa mashitaka ya kumng’oa madarakani, nchi hiyo haijawa na historia ya rais kuondolewa madarakani na Bunge la Seneti.

Kama mashitaka dhidi ya Trump yatafikishwa kwenye seneti, atakuwa ni rais wa tatu, kwani hadi sasa ni marais wawili ndio waliowahi kushitakiwa.

Rais wa kwanza kushitakiwa alikuwa Andrew Johnson mwaka 1868 na baadaye alifuatia Bill Clinton mwaka 1998.

Rais Clinton alishtakiwa kwenye seneti, Desemba 1998 kwa kashfa za kusema uwongo mbele ya mahakama kuhusu uhusiano wa kimapenzi na Monica Lewinsky.

Kashfa hii ilimshushia hadhi yake kidogo. Hata hivyo, alikuwa Rais aliyekubaliwa na raia wengi hadi mwisho wa kipindi chake. Alipoacha ikulu bajeti ya nchi ilikuwa na ziada ya pesa kwa mara kwanza tangu miaka ya 40.

Wote wawili Andrew Johnson na Bill Clinton walitakiwa kuondolewa madarakani, lakini baadaye seneti iliweza kuwaokoa na kuendelea kuwa madarakani.

Mwaka 1974, Rais Richard Nixon alipatikana akichunguza wapinzani wake kwa kashfa inayofahamika kama 'Watergate' - alijiuzulu kwa sababu alijua kuwa madai yale lazima yangemtoa madarakani na Ikulu au kuondolewa na wabunge wa seneti.

Baadhi ya watu wanadhani kuwa madai dhidi ya Rais Trump yanaweza kumuondoa madarakani, lakini kiuhalisia huu ni mwanzo tu wa hatua nyingine mbili ambazo baraza la sheria linaweza kuangazia.

Ingawa kamati kuu ambayo inangoja uchunguzi huo ilisema kuwa kama Rais atakuwa na hatia basi ataondolewa madarakani na nafasi yake itachukuliwa na makamu wa rais.

Rais Trump anashutumiwa kwa makosa ya kutumia vibaya nafasi yake ya uongozi kwa ajili ya manufaa yake binafsi ili aweze kuchaguliwa tena mwakani.

Kiongozi huyo anashutumiwa kwa kumshinikiza Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kumchunguza Joe Biden, ambaye kwa sasa ndiye mgombea aliye mstari wa mbele kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Democratic katika uchaguzi wa urais mwaka ujao, na mtoto wake wa kiume Hunter Biden, ambaye awali alifanyia kazi kampuni ya nishati ya Ukraine.

Hata hivyo, Rais Trump anasema kuwa hakuna kosa alilolifanya mpaka ifikie hatua hiyo ya kumuondoa madarakani na kuona hafai tena kuongoza.

Lakini, madai ambayo yamechochea uamuzi huu ni kuhusu taarifa iliyotolewa kuwa Trump alimpigia simu ya siri Zelensky tarehe 25 Julai.

Rais Trump alisitisha msaada wa mabilioni ya fedha pamoja na msaada kwa taifa la Ukraine na maofisa wanne waliweka wazi kuwa hatatoa fedha hizo mpaka Ukraine itakapoanza uchunguzi dhidi ya wapinzani wake, jambo ambalo ikulu ya Marekani inakanusha.

Baraza la sheria linafanya uchunguzi ambapo limeunda vikundi kadhaa na kila kundi lilikuwa linachunguza jambo lake kwa mfano masuala ya mambo ya nje, matumizi ya fedha na sheria. Kamati hizi zitawasilisha mashahidi kutoa ushuhuda kwa umma.

Kama kamati zitaamua kuwa Rais inabidi ahukumiwe basi wawakilishi wote wa Rais wanapaswa kupiga kura.

 

Chama cha Trump cha Republican kina viti 53 kati ya viti 100 vya wajumbe wa seneti na kura zinahitajika kufika robo tatu ili kiongozi huyo aweze kuondolewa kabisa katika madaraka yake.

Hivyo, kama idadi ya watu 20 kutoka chama chake wakimpinga ataondoka madarakani.

Wanaomuunga mkono Trump wanaamini kuwa upinzani unajaribu kushusha nguvu ya rais katika uchaguzi wa urais. Mlolongo huu ambao Trump anapitia umeweza kuharibu nafasi yake kama rais.

Bilionea huyu aliyeamua kuwa mwanasiasa amekuwa na maamuzi yenye utata, ikiwemo la kuingilia uchunguzi kwa madai ya Urusi kuingilia uchaguzi mwaka 2016, kukataa kutoa nakala za malipo ambayo alidaiwa kuwalipa wanawake wawili ambao walidai kuwa na mahusiano naye.