Marekani yaunga mkono maandamano Hong Kong

Wednesday November 20 2019

Washington, Marekani. Baraza la Seneti nchini Marekani limepiga kura kwa kauli moja kuunga mkono juhudi za kudai demokrasia kwenye mji wa Hong Kong.

Aidha, baraza hilo limetishia kuondoa hadhi maalum kwa mji huo kama ishara ya kuchukizwa na ukandamizaji unaondelea.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, baraza hilo pia limepitisha hatua itakayopiga marufuku mauzo ya mabomu ya machozi, risasi za mpira na vifaa vingine ambavyo vinatumiwa na maafisa wa usalama kuvunja maandamano ya umma mjini Hong Kong.

Hatua kama hiyo iliidhinishwa pia na baraza la wawakilishi la Bunge la Marekani mwezi uliopo uamuzi ambao uliikasirisha China.

Miswada hiyo miwili itaunganishwa na kuwa mmoja kabla ya kupelekwa kwa rais Donald Trump ili kutiwa saini.

Maseneta wamesema uamuzi huo unatuma ujumbe kuwa Marekani inasimama imara na bila kigugumizi kuwaunga mkono watu wa Honh Kong

Advertisement

Advertisement