Mbunge Kenya apokonywa bunduki

Muktasari:

Walinzi wa mbunge huyo ambaye ni swahiba mkuu wa Naibu Rais, Willima Ruto pia wameondolewa.

Nairobi, Kenya. Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai imemnyang’anya silaha yake mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri.

Mbunge huyo aliwasilisha bunduki yake kwa idara hiyo leo Jumanne Januari 21 baada ya Serikali kufutilia mbali leseni ya umiliki wa silaha hiyo.

Aidha, walinzi wa mbunge huyo ambaye ni swahiba mkuu wa Naibu Rais, Willima Ruto wameondolewa.

Vyanzo vya karibu kutoka kwa mbunge huyo vinasema kuwa hatua hiyo inatokana na hatua yake ya kumtetea Naibu Ruto baada ya kuzuiwa kuingia katika nyumba ya Serikali mjini Mombasa.

Mwishoni mwa wikiu mbunge huyo alihoji sababu za kiongozi huyo kuzuiliwa kuingia katika nyumba hiyo na kudai kuwa Serikali inamhangaisha.

Ilidaiwa kuwa matamshi kama haya yanaweza kuchochea fujo na uhasama katika eneo la Rift Valley.

Ngunjiri, ambaye ni mwandani wa Dk Ruto na mwanachama wa kundi la ‘Tangatanga’, alisema kuwa hatabadili msimamo wake wa kumpigia debe kiongozi huyo.

Mbunge huyo aliamriwa kurejesha bunduki yake baada ya kudadisiwa na maafisa wa DCI mjini Nakuru.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ngunjiri alisema baada ya kutoa kauli hiyo alipokea barua kutoka jeshi la polisi na kumtaka athibitishe madai yake.

 “Nashangaa ni kwa nini wananiuliza nifafanue madai yangu, ilhali habari hizo zilichapishwa magazetini hivi karibuni. Wanafaa kuwauliza wanahabari ambao walichapisha habari hizo,” alisisitiza.