Mfichua siri aibua mapya ya Boeing 787-Dreamliner

Muktasari:

Mfichua siri adai mfumo wa oksijeni wa ndege hizo una hitilafu na vipuri vyake vina kasoro.

Washington, Marekani. Mfichua siri mmoja ameibua wasiwasi baada ya kudai kuwa ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner zina matatizo ya kiufundi.

John Barnett, mfichua siri huyo, amesema kutokana na kasoro hiyo, endapo ndege itapata hitilafu ikiwa angani, huenda biria wakashindwa kupumua kwa kukosa hewa ya oksijeni.

Hata hivyo, Kampuni ya Boeing imepinga vikali madai hayo ikisema ndege zake zote zinaundwa kwa kuzingatia viwango vya usalama wa hali ya juu.

Kwa upande wake, Barnett amedai kuwa uchunguzi umebaini kuwa hadi robo ya mfumo wa oksijeni una hitilafu na huenda ikakosa kufanya kazi itakapohitajika.

Mfichua siri huyo alienda mbali na kudai kuwa hata vipuri vya ndege hiyo vina kasoro.

Kampuni hiyo imeingia katika kashfa hiyo ikiwa ni siku chache baada ya ajali mbili mbaya zilizohusisha ndege yake nyingine aina ya 737-Max katika Shirika la ndege la Ethiopia iliyotokea Machi mwaka huu na nyingine ya Lion Air ya Indonesia mwaka jana.

Barnett, ni mhandisi wa zamani wa udhibiti wa ubora, aliyefanya kazi na Boeing kwa miaka 32 hadi alipostaafu kutokana na afya yake kudorora Machi 2017.

Tangu mwaka 2010 aliajiriwa kama meneja anayesimamamia masuala ya ubora wa viwango vya uundaji ndege katika kiwanda cha Boeing cha North Charleston, Kusini mwa jimbo la Carolina.

Kiwanda hicho ni moja ya viwanda vilivyohusika na uundaji wa ndege aina ya 787-Dreamliner inayotajwa kuwa ya kisasa ya aina yake ambayo hutumika sana kwa safari ndefu kote duniani

Licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa baada ya kuanza huduma zake, ndege hiyo ilivutia mashirika kadhaa ya ndege kuimiliki na imekuwa chanzo cha faidi kwao.

Lakini Barnett (57), alidai mahitaji ya ununuzi wa ndege hiyo mpya yalisababisha uundaji wake kuharakishwa hali ambayo alisema huenda ndiyo iliyofanya viwango vya usalama wake kutozingatiwa kikamilifu.

Mwaka 2016 mfichua siri huyo aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa aligundua tatizo la kiufundi katika mfumo wa oksijeni ambao unastahili kuwasaidia abiria na marubani kupata hewa endapo ndege itakumbwa na hitilafu ikiwa angani kutokana na sababu yoyote.

Alisema mirija ya kupumulia hewa safi inatarajiwa kuning’inia kutoka juu ya ndege na kusaidia abiria kupata hewa ya oksigeni.

“Bila mfumo huo, abiria watashindwa kupumua; ikiwa ndege inapaa umbali wa futi 35,000 au juu ya bahari, abiria watazirai ndani ya dakika moja na kwenye umbali wa 40,000 watazirai ndani ya dakika 20 na ubongo kuharibika na hata kifo.”