VIDEO: Mgonjwa wa kwanza wa corona Kenya apona, aeleza alivyopata taarifa ya kuugua ugonjwa huo

Nairobi. Mtu wa kwanza kupata maambukizi ya virusi vya corona nchini Kenya amezungumza na umma kupitia video na Rais Uhuru Kenyatta akisema taarifa za kuwa na corona aliipata kupitia vyombo vya habari licha ya kuchukuliwa vipimo.
Brenda ni miongoni mwa wagonjwa watatu waliopona ugonjwa huo nchini humo amesema alisafiri kwenda Marekani Desemba mwaka jana katika miji ya Cleveland na Chicago.
Amesema baada ya hapo alisafiri kuelekea London nchini Uingereza ambapo anahisi ndipo alipopata maambukizi hayo.
Brenda ameeleza kuwa alipofika Kenya alipata kikohozi na aliamua kwenda hospitali ya Mbagathi iliyopo jijini Nairobi.
“Walinipa barakoa muda nimefika baada ya kuwaelezea nimetoka nchi za nje,” amesema Brenda.
Baada ya vipimo Brenda amesema alisikia kwenye vyombo vya habari kuwa Kenya imepata mgonjwa wa kwanza mwenye maambukizi ya virusi vya corona japo hakujua ni yeye.
“Rafiki yangu alinipigia simu akanambia huyu mgonjwa wanayemzungumzia itakuwa ni wewe nikamwambia hapana haiwezi kuwa mimi,” amesema Brenda.
Ameongeza kuwa wakati anafuatilia kwenye vyombo vya habari alisikia habari hiyo ila mtu aliyesemwa ni mtu wa miaka 27 na yeye akiwa na miaka 26.
“Nina furaha kurudi nyumbani, nimemiss jua na kuwa na uwezo wa kutoka nje,” amesema Brenda.
Mtu wa pili kupona ambaye alikuwa mtu wa tatu kuthibitishwa kuambukizwa anaitwa Brian ambaye aliambukizwa na Brenda amesema maisha ya hospitali hayakuwa mabaya.
“Nimeongea na shangazi yangu amesema sasa ataamini kuwa ugonjwa huo upo,” amesema Brian.
Kenya hadi jana Machi 31 iliripoti kuwa na wagonjwa 59 huku waliopona watatu na mmoja akifariki dunia.