Mgonjwa wa tatu wa corona Afrika aripotiwa Nigeria

Lagos. Waziri wa Afya nchini Nigeria, Osagie Ehanire ametangaza kuwepo kwa mgonjwa mmoja mwenye maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Waziri Ehanire amesema kuwa mgonjwa huyo ni raia wa Italia ambaye ni mfanyakazi nchini Nigeria alikuwa amerudi mwanzoni mwa wiki hii akitokea jijini Milan.

Amesema mgonjwa huyo ana dalili za hatari na amewekwa kwenye hospitali jijini Lagos. 

Kabla ya kuripotiwa mgonjwa huyo nchini Nigeria, kulikuwa na kesi mbili za watu waliombukizwa corona katika Bara la Afrika.

Kisa cha kwanza cha maambukizi ya corona kiliripotiwa nchini Misri ikifuatiwa na nchi ya Algeria.

Nchi nyingine zilizoripotiwa kuwa na maambukizi ya corona hivi karibuni ni pamoja na Italia, Iran na Korea Kusini.

Ugonjwa huo wa corona ambao umekuwa tishio ulianza nchini China mwaka jana mwezi Desemba na mpaka sasa ugonjwa huo umeenea kwenye zaidi ya nchi 40.