Mkuu wa Jeshi Ethiopia apigwa risasi

Muktasari:

  • Alikuwa akizuia jaribio la mapinduzi lililofanywa na watu wasiojulikana katika Serikali ya Amhara

Amhara, Ethiopia. Mkuu wa Majeshi wa Ethiopia, Jenerali Searre Mekonen anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi katika jaribio la mapinduzi ya kupindua nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Dk Abiy Ahamed amedhibitisha kiongozi huyo wa jeshi kupigwa risasi siku ya Jumamosi jioni June 22, alipokuwa akizuia jaribio la mapinduzi lililofanyika katika Serikali ya Amhara.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Abiy alisema kuwa hali ya kiongozi huyo haijulikani.

Pia, katika jaribio hilo kiongozi wa Serikali hiyo, Ambachew Mekonnen na mshauri wake, Ezez Wasie wameuawa baada ya kuvamiwa katika ofisi zao eneo la Bahir Dar na kikundi cha wanajeshi wanaodaiwa walidhamiria kufanya mapinduzi.

Hata hivyo, Abiy ambaye alizungumza kupitia televisheni ya Taifa akiwa amevaa mavazi ya kijeshi alisema Serikali imefanikiwa kudhibiti mapinduzi hayo.

Kiongozi huyo wa Serikali ya Ethiopia alilaani vikali tukio hilo na kusema kuwa wau kadhaa wanashikiriwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo

Tukio hilo limetokea ikiwa ni muda mchache baada ya ubalozi wa Marekani nchini humo kutoa tahadhari kufuatia milio ya risasi katika mji mkuu wa Addis Ababa pamoja na vurugu karibu na mji mkuu wa jimbo la Amhara, Bahir Dar.

Mara kwa mara Ethiopia imekuwa ikikabilia na migogoro ya kikabila na kusababisha mapigano jambo lilosababisha nchi hiyo kushindwa kutawalika.

Hata hivyo, mwaka 2018 wananchi wa Ethiopia walimchagua  Dk Abiy kuwa waziri mkuu ambaye kwa kiasi kikubwa ameweza kuleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuwaachia wafungwa wa kisiasa, kuboresha uchumi, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kupambana na vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.