Moi alivyomaliza miaka 24 madarakani bila mke

Rais mstaafu wa Kenya, Daniel Arap Moi anazikwa leo nyumbani kwake Kabarak, Nakuru nchini Kenya. Kiongozi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 95 alifariki dunia Februari 5 katika hospitali ya Nairobi alikokuwa amelazwa kwa takribani miezi mitatu.

Moi anazikwa akiwa na rekodi ya kuwa rais pekee wa Kenya aliyekaa madarakani kwa muda mrefu wa miaka 24, baada ya kupokea kijiti hicho kutoka kwa mwasisi wa Taifa hilo, Jomo Kenyatta alipofariki dunia mwaka 1978.

Licha ya kuitwa dikteta na wakosoaji wake, Moi alikuwa akipendwa na wananchi wake. Hata hivyo, katika utawala wake, wapinzani hawakupata nafasi, baadhi yao waliwekwa kizuizini na hata wengine kuuawa.

Moi alihakikisha hakuna mtu anamyumbisha katika utawala wake. Aliwadhibiti wapinzani na wote waliokuwa tofauti naye. Alifuta mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1982 kabla ya kuviruhusu tena mwaka 1991.

Utawala wake wa miaka 24 ulijaa chungu na tamu kwa Wakenya. Siku anaondoka madarakani Desemba 2002, baadhi ya watu walifurahi kwa sababu walikuwa wamemchoka. Hata hivyo, anakumbukwa kwa kujenga mfumo imara wa elimu nchini humo.

Wakati wa utawala wake, Moi alifahamika kwa majina mengi, baadhi ya majina hayo ni kama vile Mtukufu Rais, Nyayo na Rais kwa bahati mbaya (accidental president). Alipenda kutukuzwa na mara nyingi kuonekana kwenye vyombo vya habari.

Pia, atakumbukwa kama mmoja wa viongozi walioifufua jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2000, akiwa pamoja na viongozi wenzake wa nchi wanachama – Benjamini Mkapa wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda.

Hakuingia madarakani kirahisi

Januari 1967, Mzee Kenyatta alimteua Moi kuwa Makamu wa Rais akiwa na umri wa miaka 43. Moi alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Joseph Murumbi ambaye alijiuzulu nafasi hiyo.

Baada ya kufariki kwa Kenyatta mwaka 1978, Moi alikuwa ndiyo mrithi halali wa kiti cha Rais kwa mujibu wa Katiba ya Kenya. Hata hivyo, genge la watu wa karibu wa Kenyatta walitaka kumnyang’anya haki hiyo.

Genge hilo halikutaka Moi awe Rais. Alilifahamu hilo na kuhisi maisha yake kuwa hatarini, hivyo alipopata taarifa za kifo cha Kenyatta, Moi aliikimbia nyumba yake ya Rift Valley na kurejea baada ya kuhakikishiwa usalama wake.

Kundi hilo lilitaka kubadilisha hata Katiba ya Kenya ili mradi kutomruhusu Moi kuwa Rais. Hata hivyo, hawakufanikiwa kwa sababu Moi alitambua njama zao na

kujilinda mpaka alipoapishwa kuwa Rais.

“Hakuna mtu aliyejua kwamba atakaa madarakani kwa muda mrefu. Alikuwa Rais aliyeweza kuziba pengo,” anasema mwanahistoria kutoka chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya, Lydia Muthuma kama alivyonukuliwa na shirika la habari la Al Jazeera.

Baada ya kuingia madarakani, Moi alionekana kama alama ya kuiunganisha Kenya, hata hivyo, mfumo wake wa uongozi ulibadilika baada kupona katika jaribio la mapinduzi ya mwaka 1982, akawa dikteta halisi.

Jaribio la mapinduzi

Tukio la Agosti 1, 1982 litabaki kuwa siku mbaya katika historia ya Kenya na siku hiyo ndiyo iliyombadilisha Moi katika utawala wake, akiwa amekaa madarakani miaka minne tangu alipoapishwa kuwa Rais.

Jaribio hilo lilitekelezwa na wapinzani wake pamoja na baadhi ya maofisa wa kikosi cha jeshi la anga kwa madai kwamba utawala wa Moi ulijaa ukabila, ufisadi na rushwa. Waliomba msaada wa wananchi katika mapinduzi hayo lakini hawakufanikiwa.

“Baada ya jaribio la mapinduzi kukwama, tuliuona uhalisia wa Moi. Alitufanya tuelewe nani alikuwa anahusika. Taarifa ya habari ilianza kwa alichokifanya siku hiyo. Hakuwa kiongozi mvumilivu,” anasema Muthuma.

Mwaka 1982, serikali ya Moi ilifanya mabadiliko ya Katiba kupitia Bunge na kuifanya Kenya kuwa nchi ya chama kimoja.

Wakati Jeshi la nchi hiyo linadhibiti jaribio la mapinduzi hayo, watu 159 walikufa katika mapambano hayo.

Serikali ya Moi ilisimama imara katika kushughulikia utovu wa nidhamu, hii ni kwa mujibu wa Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano ambayo iliufanyia tathmini utawala wa Moi.

Wanasiasa na wanaharakati wengine waliothubutu kuupinga utawala wa Moi waliwekwa kizuizini na kuteswa bila kufikishwa mahakamani, ripoti hiyo inaeleza matukio ya kuwekwa kizuizini na mauaji yakiwamo mauaji ya Waziri wa Mambo ya Nje, Robert Ouko.

“Mahakama ilikuwa ikiisaidia Serikali katika ukiukaji wa sheria, wakati Bunge lilibadilishwa kuwa chombo cha kuwadhibiti vibaraka kwa msaada wa serikali,” ripoti hiyo ya Tume ya maridhiano inabainisha.

Alivyoondoka madarakani

Mwaka 2002, Moi alistaafu urais baada ya kupata shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi ambao hawakutaka aongeze muhula mwingine. Pia, ndani ya chama chake cha Kanu hakuwa na mvuto tena wa kugombea kwa sababu katiba haikumruhusu.

Alitumia ushawishi wake kumteua Uhuru Kenyatta kama mgombea wa urais wa chama cha Kanu, jambo lililozusha minong’ono kutoka kwa wanasiasa wengine waliokuwa wanawania nafasi hiyo, jambo hilo liliwafanya wanachama wengi kuachana na Kanu.

Hatua ya kumchagua Kenyatta ilionekana na wengi kama ya upendeleo na kama mbinu tu ya kumfanya Moi aendelee kuitawala Kenya hata baada ya kustaafu.

Ilionekana anataka Uhuru aweze kuyaficha yale mabaya aliyoyafanya wakati wa uongozi wake.

Hata hivyo, Kenyatta hakushinda katika uchaguzi huo badala yake Mwai Kibaki ndiyo akachaguliwa. Kenyatta alikubali matokeo na kuwa kiongozi wa upinzani bungeni huku akikiongoza chama cha Kanu.

Moi aliondoka madarakani na kuiacha Kenya ikiwa na ukuaji hasi wa uchumi, licha Taifa hilo kuwa na maendeleo makubwa Afrika Mashariki. Alizilaumu nchi za Magharibi kwa kuzitangaza vibaya nchi za Afrika na kwa ugumu wa maisha kwa Wakenya.

Azima ndoto ya Ruto

Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto anasimulia jinsi alivyoingia kwenye mgogoro na Moi baada ya kutangaza kuwania urais. Anasema Moi hakutaka agombee nafasi hiyo na mara kadhaa alikuwa akimdhihaki hadharani.

“Alitamka maneno ya kudhalilisha mno tangazo langu, akipuuza azma yangu na kusema nilikuwa ninapotosha jamii. Moi alijitokeza na kusema Ruto hawezi kuwa kiongozi, mnapaswa kuchagua watu wenye ujuzi kama Henry Kosgei na Nicholas Biwott. Ninakumbuka wakati huo nikifafanua kwamba, sikutaka kuwa kiongozi wa jamii bali, niliazimia kuwa Rais,” anasema Ruto akisisitiza nia yake.

Maisha yake ya familia

Moi alizaliwa Septemba 2, 1924 katika kijiji cha Kurieng’wo kilichopo katika Kaunti ya Baringo. Alipewa jina na baba yake Kimoi Arap Chebii ambaye alikuwa mfugaji. Walikuwa wakiishi katika milima ya Tugen ili kuepusha kuingiliana na Wamaasai katika karne ya 19.

Alikuwa ni mtoto wa tano wa mke mkubwa wa baba yake – Chebii. Alipewa jina la Toroitich ambalo maana yake ni “karibisha ng’ombe nyumbani”, ikionyesha jinsi gani ng’ombe walivyokuwa muhimu katika maisha yao.

Akiwa na umri wa miaka minne, baba yake alifariki dunia na kaka yake mkubwa, Tuitoek akawa kiongozi wa familia hiyo. Tuitoek alikuwa na ushawishi mkubwa katika kumfanya Moi aende shule katika umri mdogo kama njia ya kuepuka umasikini na dhuluma wakati wa utawala wa wakoloni.

Moi alifunga ndoa na Helena (Lena) Bommet mwaka 1950 na walijaliwa watoto wanane; wa kike watatu na wa kiume watano; wa kike ni Jennifer, Doris na June ambaye aliasiliwa; wa kiume ni Jonathan, Raymond, John Mark, Philip na Gideon.

Hata hivyo, Moi alitengana na mke wake mwaka 1974 na talaka yao kukamilika mwaka 1979. Moi aliendelea kuishi na watoto wake huku akipambana kujiimarisha kisiasa hasa kutokana na kudhalilishwa kwake na wafuasi wa Mzee Kenyatta.

Moja ya sababu za kutengana na mkewe inatajwa kuwa ni kitendo cha Lena kukataa kucheza muziki na Mzee Kenyatta katika hafla moja ya Ikulu, wakati Moi alikuwa akicheza na Mama Ngina Kenyatta.

Kitendo hicho kilionekana kuwa fedheha kwa Moi, jambo lililomfanya atengane na Lena. Lena alikuwa Mkristo ambaye alikuwa na dhana kwamba kucheza muziki ni dhambi, hivyo, hakuwa tayari kufanya hivyo.

Katika kipindi chote, Lena hakuonekana hadharani mpaka Julai 2004 alipofariki dunia. Awali, ilifahamika kwamba angezikwa Sacho lakini ikabadilishwa akazikwa Kabarak mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi Moi.

Kifo cha Lena kilimuunganisha tena na mume wake. Alikuwa mke wa rais ambaye Wakenya hawakuwahi kumfahamu.