Mtuhumiwa afa kortini

Muktasari:

Alikuwa akikabiliwa na tuhuma za mauaji ya binamu yake ambako alianguka ghafla na kufariki dunia.

Mbale, Uganda. Mkazi wa Kijiji Buyobo, nchini Uganda, Simon Mayuya amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla mahakamani.

Mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 54 alifikwa na mkasa huo leo Januari 21 katika Mahakama Kuu nchini Uganda wakati kesi yake ilipokuwa imekuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Kwa mara ya kwanza Mayuya alifikishwa mahakamani hapo miezi sita iliyopita akikabiliwa na tuhuma za jaribio la kumuua binamu yake na kurejeshwa rumande katika Gereza la Maluku.

Mwanasheria wa Mayuya, David Moli alisema mteja wake alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya uti wa mgongo kutokana na kunusurika kwenye ajali ya gari aliyopata kabla ya kukamatwa na kuwekwa rumande

Moli aliongeza kuwa kabla hali ya mteja wake kubadilika aliiomba Mahakama kumpa dhamana ili apelekwe hospitali kupatiwa matibabu kabla ya kurejea tena gerezani.

“Leo tulitakiwa kuwapo mahakamani kwa ajili ya kusikiliza maombi ya dhamana lakini nimeshtushwa kusikia mteja wangu ameanguka na kugonga kichwa chake kwenye kiti na kupoteza maisha,” alisema.

Mtoto wa marehemu, Tom Wetaka alisema kuwa baba yake alianguka na kugonga kichwa kwenye kiti kilichokuwa kinakaliwa na mmoja wa walinzi wa watuhumiwa.

 “Baba yangu alikuwa anaumwa na tayari hali yake ilikuwa imedhoofika. Alikuwa hawezi kutembea vizuri peke yake bila msaada. Walinzi wa wafungwa walikuwa wanamlazimisha kukimbia kama wengine, ndiyo maana alikosa nguvu na kuanguka,” alisema.