Museveni ataka wenye nyumba wawasamehe kodi wapangaji

Muktasari:

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewataka wamiliki hao wa nyumba kuwa wavumilivu maambukizi ya virusi vya corona yatakapokwisha.

Kampala, Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amepiga marufuku wamiliki wa nyumba kuwafukuza wapangaji watakaoshindwa kulipa kodi wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Rais Museveni ametoa amri hiyo wakati akihutubia taifa hilo na kutoa taarifa ya hali ya maambukizi ya virusi vya corona.

Museveni aliwataka wamiliki wa nyumba wawe wavumilivu kwa kuwa janga la corona linamuathiri kila mmoja.

Alisema kitendo cha wamiliki wa nyumba kuwafukuza wapangaji wanaoshindwa kulipa kodi hakikubaliki.

Wiki iliyopita Rais Museveni alitangaza amri ya kutotoka nje na kusalia nyumbani kwa siku 14 kuanzia 1.000 usiku hadi 12.00 asubuhi.

Pia, Rais Museveni alipiga marufuku watu kuendesha magari yao isipokuwa ya kusafirisha mizigo na kutokufunguliwa kwa maduka na kuruhusu biashara ya vyakula pekee.

Mapema wiki iliyopita serikali ya nchi hiyo ilianza kutoa msaada wa chakula kwa familia zilizoathirika zaidi na agizo la kusalia nyumbani.

Rais Museveni alisema mpaka jana jioni nchi hiyo ilikuwa na wagonjwa wenye maabukizi ya virusi vya corona 53.