Museveni kutembea siku sita msituni kukumbuka vita vya ukombozi

Kampala. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni leo Jumamosi ameanza ziara ya siku sita msituni kupitia njia aliyotumia katika vita kabla ya kuchukua serikali kwa njia ya mapinduzi miaka 30 iliyopita.

Hata hivyo, wakosoaji wamekuja juu wakisema hana lolote zaidi ya kushawishi uungwaji mkono katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Museveni ni miongoni mwa marais wa muda mrefu barani Afrika, tangu alipochukua madaraka mwaka 1986 baada ya kuongoza vita vya msituni kupinga utawala wa Idi Amini na Milton Obote, na anatarajia kuomba awamu ya sita katika uchaguzi ujao.

Ameanza ziara hiyo ya kilometa 195kwa mguu kutoka Galamba, kaskazini mwa Kampala na itakamilika Januari 10 katika eneo la Birembo kusini mwa jiji hilo, ambako majeshi yake yalikabiliwa na upinzani mkali kabla ya kuiangusha Serikali ya Obote.

“Safari hii muhimu imeanza leo na itachukua siku sita. Hii ni safari ambayo rais anaongoza,  ni kumbukumbu ya mambo yaliyopita ili kufurahia yaliyopo,” amesema ofisa habari mwandamizi wa Rais Museveni.

 

“Ziara itachukua siku sita msituni, njia ya ukombozi iliyoongozwa na Museveni katika ukombozi wa nchi.”

 

Ziara hiyo imekuja baada ya mwezi mmoja tangu rais huyo afanye matembezi mengine katika Jiji la Kampala ya kupiga vita ufisadi, hatua inayopingwa na wakosoaji wake wakisema rushwa ilianza katika utawala wake.

Museveni akabiliwa na upinzani katika uchaguzi kutoka kwa mwanamuziki na mwanasiasa maarufu, Bobi Wine, ambaye anasema mbele ya vijana kuwa katika maisha yake amemjua rais mmoja tu.

“Haya matembezi ni sehemu ya kampeni ambazo hazina maana zinazofanywa na Serikali kutafuta uungwaji mkono wa Museveni miongoni mwa Waganda,” alisema Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi.

“Ushauri wangu ni kwamba badala ya kutumia kodi za Waganda kwa ziara za namna hiyo, Museveni anatakiwa kufahamu kuwa muda wake wa kuacha madaraka umewadia. Muda wa kuwadanganya wakulima umempita. Wananchi wanataka mabadiliko, na si zaidi ya hapo,” alisema.