Mwanaume anayedaiwa kuanguka kutoka kwenye ndege apatikana akiwa hai

Muktasari:

Mtu huyo anadaiwa kuanguka kutoka kwenye ndege ya Kenya Airways.

Nairobi, Kenya. Mwanaume anayekisiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 30 aliyeanguka na kufariki dunia kutoka kwenye ndege ya Kenya Airways mjini London Uingereza amepatikana akiwa hai.

Mwanaume huyo ambaye picha ya mchoro wake ilionekana katika uchunguzi wa hivi karibuni akiwa amejificha ndani ya ndege amebainika kuwa hai, akiwa kwenye gereza la Kenya.

Mamlaka ya Magereza nchini Kenya ilimtaja mwanaume huyo kwa jina la Cedric Shivonje Isaac ambaye amekuwa akishikiliwa tangu mwezi Agosti na si Paul Manyasi, ambaye alitambuliwa katika taarifa ya Sky News.

Uchunguzi wa Shirika la habari Sky News wiki hii ulithibitisha mchoro wa sura ya mtu huyo na kutoa picha yake hadharani.

Ripoti hiyo ilionyesha sura ya mwanaume ambaye Sky News iliambiwa kuwa alifanya kazi kwenye kampuni ya usafi kwenye uwanja wa ndege na anayedaiwa kujificha kwenye eneo la chini ya gia ya ndege.

Lakini baadaye ilibainika kuwa mwanaume aliyeonekana kwenye picha hizo yuko hai na amekuwa akishikiliwa na polisi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Baba wa mwanaume huyo amekana kauli yake alipozungumza na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la BBC na sasa anasisitiza mtoto wake bado yuko hai. Awali baada ya kutolewa kwa mchoro huo, baba huyo alikiri mtoto wake amekufa.

Haijajulikana mkanganyiko huu umetokea vipi lakini wapelelezi wanajaribu kutafuta uwezekano kati ya Isaac, mtu aliye kwenye picha na Manyasi, mwanaume aliyetambuliwa kwenye ripoti.

Taarifa ya kupatikana kwa mtu huyo imezua maswali mapya kuhusu uwezo wa mamlaka za Kenya kumbaini mtu aliyeingia ndani ya ndege hiyo ikiwa miezi minne tangu alipoanguka kutoka kwenye ndege ya Kenya Airways kuelekea kwenye Uwanja wa ndege wa Heathrow jijini London.

Sky News wanasema walipata kidokezo cha kwanza kutoka kwa dereva wa teksi za Uber kwa jina Kamau aliyewajulisha kwamba yupo mfanyakazi wa kampuni ya kufanya usafi ya Colnet aliyetoweka kipindi hicho huku baadhi ya wafanyakazi walizungumzia kutoweka kwa mfanyakazi huyo.

Inaelezwa kuwa baadaye walikutana na mwanamke mfanyakazi wa Colnet ambaye hakutaka kutambuliwa aliyewaambia kwamba mwenzake kwa jina Paul Manyasi alitoweka mwishoni mwa mwezi Juni.

“Mara ya mwisho kumuona tulikuwa kazini, ghafla akatoweka, hakuna aliyejua alikoenda,” mwanamke huyo aliwaambia waandishi wa BBC.

Anasema baada ya taarifa hiyo, siku iliyofuata asubuhi kiongozi wao aliwaambia kuna aliyekuwa ametoweka lakini hawakuwa wanajua ni nani hasa na kwamba jambo hilo linafaa kuwa siri kwanza.

Mwanamke huyo aliyekuwa na picha za Paul alidai alikuwa na uhusiano naye wa miaka miwili na walikuwa na mpango wa kuoana.

Inaaminika kuwa Paul alikuwa akiishi mtaa wa Mukuru kwa Njenga pamoja na rafiki yake Patrick ambaye ndiye aliyemsaidia kupata kazi. Wawili hao wanatokea jimbo moja Kakamega.

Alipohojiwa kuhusu mkasa huo, Patrick alisema rafiki yake Paul alikuwa na ndoto ya kuondoka Kenya lakini hakuwahi kufichua alitaka kwenda wapi na ni kazi gani angeenda kuifanya.