Mwanga waanza kuonekana Sudan; jeshi, wapinzani waunda serikali ya pamoja

Muktasari:

  • Taarifa ya Jeshi la Sudan ilisema kuwa utawala huo wa pamoja unatarajiwa kuongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu.

Khartoum, Sudan. Hatimaye viongozi wa kijeshi nchini Sudan wameunda Baraza huru la pamoja na muungano wa makundi ya upinzani.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, Baraza hilo lililotangazwa leo Jumatano Agosti 21 mjini Khartoum litaongoza nchi hiyo kurudi kwenye utawala wa kiraia.

Kutangazwa kwa Baraza hilo kunafuatia pande hizo mbili kutiliana saini makubaliano ya kunda Serikali mseto katika fhafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Taarifa ya Jeshi la Sudan ilisema kuwa utawala huo wa pamoja unatarajiwa kuongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu.

Awali mara baada ya kiongozi wa nchi hiyo Dk Omar al Bashir kupinduliwa, jeshi la nchi hiyo lilitangaza Baraza la Kijeshi la Mpito (TMC)  jambo lilopingwa na waandamanaji waliokuwa wakidai utawala wa kiraia.

Katika maandamano hayo zaidi ya watu 100 wakiwamo wanafunzi watano walifariki dunia baada ya jeshi la nchi hiyo kuwafyatulia risasi za moto

Taarifa ya jeshi hilo ilisema Baraza hilo lenye wajumbe kumi na moja, linatarajiwa kuongozwa na Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan ambaye awali alikuwa kiongozi wa Baraza la Kijeshi la Mpito (TMC).

“Baraza litakuwa na wajumbe sita kutoka upande wa raia na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi watano,” ilifafanua taarifa hiyo.

Habari zaidi zinasema kuwa baadaye baraza hilo litamuapisha Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye anatarajiwa kutoa miongoni mwa wajumbe hao.

Makubaliano hayo yalijumuisha uundwaji wa baraza huru na kupokezana kijiti cha uongozi wa baraza baina ya jeshi na wapinzani ambako mwishoni mwa muda wa uongozi wao, baraza hilo linarajiwa kuandaa uchaguzi huru utakaorejesha utawala wa kiraia.

Jenerali Mohamed Hamdan Hemeti Dagolo, ambaye anatajwa kuwa ndiye mtu mwenye nguvu zaidi kwa sasa nchini Sudan ameahidi kuheshimu makubaliano hayo.