Ndege za abiria kutoka China kutua Kenya

Muktasari:

Kenya imesema itaendelea kupokea ndege za abiria kutoka China licha ya nchi hiyo ya barani Asia kukumbwa na maambukizi ya virusi vya corona vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 2,300.

Dar es Salaam. Kenya imesema itaendelea kupokea ndege za abiria kutoka China licha ya nchi hiyo ya barani Asia kukumbwa na maambukizi ya virusi vya corona vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 2,300.

Ndege hizo zitakazobeba  wataalam, wafanyakazi na wafanyabiashara kutoka China zinatarajiwa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Uamuzi huo umekosolewa na raia wa Kenya kwa maelezo kuwa Serikali ya nchi hiyo ilikataa kuwarudisha wanafunzi waliopo China.

Jana Jumatano Februari 26, 2020 ubalozi wa China nchini Kenya ulithibitisha kuwa Shirika la ndege la China  limeamua kuendelea na safari ya moja kwa moja kutoka Guangzouh hadi Nairobi, Kenya.

Taarifa zaidi zinaeleza kutakuwa na safari moja kwa wiki hadi Machi 25, 2020 na ubalozi umeieleza Kenya kufanya ukaguzi na kuwapima wasafiri wote watakapowasili.