Ngoma bado ‘nzito’ kwa Rais Trump, apambana mahakamani kujinasua asing’olewe madarakani

Rais wa Marekani, Donald Trump

Muktasari:

Ushahidi watolewa kuwa alihusika moja kwa moja kupiga simu Ukraine kushinikiza uchunguzi wa Biden, Pia mahakama imeamuru rekodi zake za kodi zichunguzwe.

Washington, Marekeni. Hali inazidi kuwa mbaya kwa Rais wa Marekani, Donald Trump huku mwenyewe akihaha kujinasua katika mtego wa kung’olewa madarakani.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Uingereza (AFP), balozi Davis Holmes ambaye alisikiliza mazungumzo baina ya kiongozi huyo wa Marekani na Rais wa Ukraine natarajiwa kutoa ushahidi wake ili kufanikisha uchunguzi huo.

Tayari mabalozi wawili wa Marekani wametoa ushahidi mzito, yakiwamo maelezo mapya kuhusu juhudi za Rais huyo kuitaka Ukraine kumchunguza mshindani wake katika uchaguzi wa 2020, Joe Biden.

Ushahidi huo umetolewa na kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni, kuanzia juzi Jumatano katika kamati ya Bunge inayoendesha uchunguzi wa dhidi ya Trump.

Hata hivyo, Rais Trump amepuuza uchunguzi huo unaosimamiwa na Bunge linaoongozwa na Chama cha Democrats, kuwa ni “kutafuta mchawi” na kuwa ana kazi nyingi hivyo hawezi hata kufuatilia mahojiano hayo. Ameungwa mkono na wabunge wa chama cha Republican.

William Taylor, ofisa wa juu wa Ubalozi wa Marekani nchini Ukraine, alianza kutoa ushahidi wake mbele ya Kamati ya uchunguzi akieleza masuala mapya kuhusu juhudi za Trump kushinikiza Ukraine, hoja ambayo ndiyo msingi katika mchakato huo wanne, wa kutaka kumng’oa rais katika historia ya Marekani.

Chama cha Democrats kinamtuhumu Trump kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kutumia msaada wa kijeshi na Ikulu ya White House, kumshinikiza Rais Volodymyr Zelensky kufungua upelelezi dhidi ya Biden na mwanaye Hunter.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo machachari jana aliwasilisha pingamizi lake katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufani nchini humo kutoa ruksa kwa Bunge kuagiza nyaraka zake kodi za karibu miaka 10 kwa ajili ya ukaguzi.

Uamuzi huo umezima juhudi za Trump ambaye amekuwa akipambana kuhakikisha rekodi zake za kibiashara haziangukii mikononi mwa wapinzani wake wa Democrats.

Kijana huyo wa Biden alifanya kazi katika bodi ya kampuni moja ya gesi nchini Ukraine iitwayo Burisma.

Ushahidi muhimu ni maelezo ya simu ya Ikulu ya Julai 25 kati ya Trump na Zelensky ambapo Trump anamtaka mwenzake wa Ukraine amchunguze Biden.