Ni kweli Netanyahu anahofia kufungwa jela kama mtangulizi wake Ehud Olmet?

“Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha.” Msemo huu unaweza kuwa na tafsiri mbili kwa Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu anayekabiliwa na mambo makuu kadhaa.

Waziri Mkuu huyo mwenye umri wa miaka 69 alitarajia matokeo ya uchaguzi yangeleta historia kwake kwa maana angekuwa waziri mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, akimzidi Baba wa Taifa hilo, David Ben-Gurion ambaye ni waziri mkuu wa kwanza wa Israeli.

David Ben-Gurion alianza kuwa waziri mkuu mwaka 1948 hadi 1954 kupitia chama cha Mapai na alirudi tena kwenye wadhifa huo mwaka 1955 hadi 1963. Netanyau kwa mara ya kwanza alikuwa waziri mkuu mwaka 1996 hadi 1999 kupitia chama cha Likud na alirudi kwenye wadhifa huo tena mwaka 2009 hadi sasa.

Mbali na kuweka historia ya kukaa madarakani kwa muda mrefu, kiongozi huyo anakabiliwa na tuhuma za ufisadi na uvunjaji wa haki na sheria za nchi.

Hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona Netanyahu hana namna nyingine ya kupata kinga ya kutoshtakiwa kwa ufisadi zaidi ya kuendelea kuwa waziri mkuu.

Pigo kwa Netanyahu lilianza kwenye ushindi mwembamba alioupata kwenye uchaguzi wa Aprili na kushindwa kuunda serikali ya mseto na kiongozi wa upinzani wa chama cha Blue and White, Benny Gantz ambaye tayari ametamka kwamba chama chake kipo tayari kuungana na chama tawala cha Likud ikiwa kitaongozwa na kiongozi mwingine.

Gantz anasisitiza kuwa hawataki kujihusisha na Netanyahu ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ulaji rushwa na utumiaji mbaya wa madaraka.

Kutokana na vyama hivyo kushindwa kuunda serikali ya mseto wapiga kura wa Israeli walilazimika kushiriki katika uchaguzi mkuu wa pili uliofanyika Septemba 17. Upinzani ulichukulia hiyo ni njama ya kiongozi huyo kutaka kung’ang’ania madaraka kwa kuwalazimisha wabunge wenzake kulivunja Bunge ili uchaguzi mpya uitishwe na kwamba angeweza kuongeza ushawishi ili ashinde uchaguzi.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, David Monda akiwa Johannesburg nchini Afrika Kusini anasema sababu za Netanyahu kushindwa kuunda serikali mpya zilitokana na namna alivyokuwa akifikiri kwamba bado wananchi wa Israeli wanampenda na atashinda uchaguzi ili awe waziri mkuu aliyetawala kwa muda mrefu kumpita Baba wa Taifa, David Ben-Gurion.

Netanyahu hakuwa na namna nyingine zaidi ya kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi mwingine uliofanyika Septemba 17.

Hata hivyo, haikuwa suluhu kwake kwani amepata viti 31 dhidi ya mpinzani wake aliyepata viti 33. Bunge lina jumla ya viti 120 na ili chama kiweze kuunda serikali kinatakiwa kupata angalau viti 61.

Wakati hadi hivi sasa hakuna aliyeibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa Israeli, Netanyahu amemtaka mpinzani wake mkuu Gantz washirikiane kuunda serikali ya mseto.Katika ujumbe wa picha za video, Netanyahu amesema ni matumaini yake ya kuunda serikali ya mrengo wa kulia hayapo tena kutokana na matokeo ya uchaguzi.

Ametoa wito wa kumtaka Gantz ashirikiane naye mara moja ili kuunda “serikali pana ya umoja wa kitaifa.”

Gantz mwenye mrengo wa kati wa chama cha Blue and White, amesema hatoungana kuunda serikali ya umoja hadi Netanyahu aondoke kwenye uongozi wa chama cha Likud.

Hoja ya vyama vingine

Avigdor Lieberman anaonekana ni mwenye nafasi yenye nguvu zaidi kutokana na kukosekana chama cha walio wengi.

Lieberman ambaye ni kiongozi wa chama kinachojulikana kama Yisrael Beytenu (Israel ni Nyumbani Kwetu) amerejea mara kadhaa kusema anapendelea kuwepo serikali ya umoja ambayo itamaanisha serikali itakayo kuwa na chama cha Gantz cha Blue and White, Chama cha Netanyahu Likud, na chama chake.

Kesi inayomkabili Netanyahu

Jeshi la Polisi nchini Israeli liliwahi kupendekeza kuwa Netanyahu na mkewe Sara wafunguliwe mashtaka kwa tuhuma za ulaghai, ufisadi na kuvunja uaminifu na tayari kumekuwa na shinikizo kuwa lazima ajiuzulu.

Polisi katika uchunguzi wao wamegundua kuna ushahidi wa msingi kufungua kesi dhidi ya waziri mkuu na mkewe juu ya tuhuma hizo.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa Netanyahu na mkewe walishiriki kuipendelea kampuni kubwa ya mawasiliano ili nao waandike habari zenye upendeleo kuhusu waziri mkuu kupitia kampuni tanzu ya habari, Bezeq, kwenye tovuti yao inayo julikana kama, Walla.

Kesi hiyo inahusu kushukiwa kwa wasiri wake Netanyahu walioshiriki kuandaa kanuni zenye kuipendelea kampuni ya mawasiliano ya Bezeq katika biashara yenye thamani ya mamilioni ya dola za Kimarekani.

Polisi tayari wamependekeza Netanyahu kufunguliwa mashtaka juu ya tuhuma za ufisadi katika kesi nyingine mbili.

Moja inahusu Netanyahu kupokea zawadi za mabilioni ya fedha kutoka kwa marafiki na ya pili inahusu madai ya kupitisha sheria yenye upendeleo kwa gazeti moja kwa makubaliano liandike habari nzuri kuhusu Netanyahu.

Hata hivyo, waziri mkuu huyo amekanusha kufanya kosa lolote, akitupilia mbali tuhuma hizo na kuziita ni kutafuta mchawi na anadai kuwa kampeni hiyo ya kumchafua inaendeshwa na vyombo vya habari.

Mwanasheria mkuu nchini Israeli sasa ataamua iwapo afungue mashtaka kuhusu madai hayo.

Netanyahu amesema: “Pendekezo hili la polisi dhidi yangu na mke wangu halimshangazi mtu yeyote, mapendekezo haya yalishakuwa yameamuliwa na yalivuja hata kabla ya uchunguzi kuanza.”

“Nina imani kuwa katika kesi hii, mamlaka zinazo chunguza suala hili zitafikia uamuzi kuwa hakuna chochote kwa sababu hakuna ushahidi,” anasema Netanyahu.

Vyombo vya habari nchini Israeli vinasema kuwa wachunguzi wamemhoji Netanyahu mara kadhaa.

Akataa kujiuzulu

Netanyahu ambaye yuko kwenye madaraka kwa muda mrefu sasa amekataa shinikizo la kujiuzulu linalotokana na mwendelezo wa kashfa ya ufisadi.

Amesema serikali yake iko imara, siku moja baada ya polisi kutoa pendekezo la yeye kushtakiwa kwa kesi mbili za ufisadi.

Netanyahu ameeleza kuwa madai hayo ya ufisadi ni yenye “kumkandamiza, yamevuka mipaka na kuna dosari nyingi kama vile ilivyo jibini ya Uswisi” na kuahidi kuendelea na uongozi wake. Polisi wametuhumu Netanyahu kwa kupokea rushwa na kukiuka dhamana aliyopewa kwa kumhusisha na kashfa mbili za ufisadi na wanasema kuna ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka.

Wapelelezi wa polisi wamedai kuwa Netanyahu alipokea takriban dola za Marekani 300,000 kama zawadi kutoka kwa mabilionea wawili, zikiwemo aina ya sigara kutoka Cuba “cigars”, ulevi aina ya champagne na mapambo aliyopokea kinyume cha sheria.

Pia, imedaiwa kuwa alifikia makubaliano na mchapishaji wa magazeti wa Israeli kwa ajili ya kuwataka wachapishe habari zenye upendeleo kwake. Na hivyo, polisi wanasema kuwa aliahidi kusimamia maslahi yao watakapomsaidia katika kuzuia kashfa hiyo isichapishwe.

Viongozi wa upinzani nchini Israeli wanataka Netanyahu ajiuzulu, wakisema kuwa ni fisadi na hafai kuliongoza taifa.

Ahofia yaliyomkuta Ehud Olmet

Wachambuzi wanasema huenda Netanyahu anahofu ya kufungwa jela kama akakutwa na hatia ya madai ya rushwa na ufisadi. Hofu ya Netanyahu inatokana na yaliyomkuta mtangulizi wake, waziri mkuu wa zamani, Ehud Olmet, ambaye alihukumiwa kifungo cha miezi 19 jela kwa makosa ya ufisadi na kuzuia kutenda haki.

Olmert ni kiongozi wa kwanza kutoka ngazi za juu kutiwa mbaroni. Akiwa na umri wa miaka 70 alifungwa katika gereza la Ma’asiyahu lililopo Ramle nchini humo. Olmert alikuwa waziri mkuu wa Israeli kuanzia mwaka 2008 hadi 2009.

Olmert alitenda makosa hayo ya ufisadi na kuzuia mkono wa sheria kufanya kazi yake, wakati huo akiwa waziri wa biashara nchini humo. Olmert ni kiongozi wa kwanza aliyetumikia cheo cha uwaziri mkuu kufungwa jela huko Israeli.

Matokeo yalivyotangazwa

Matokeo ya baada ya kufungwa vituo vya kura yaliotolewa na shirika la utangazaji Israeli Kan yakionyesha kuwa chama cha Blue and White huenda kingejinyakulia viti 32 na chama cha Likud kikajipatia viti 31 kati ya jumla ya viti 120 bungeni.

Katika nafasi ya tatu ni chama cha Israeli Arab Joint List kilichojinyakulia viti 13; kikifuatwa kwa chama cha Lieberman, Yisrael Beitenu kilichojinyakulia viti tisa; Vyama vya Shas na cha umoja wa Torah Judaism vikijinyakulia viti tisa kila mmoja; cha mrengo wa kulia Yamina viti saba, Labour-Gesher viti vitano na Democratic Union Alliances kilipata viti sita.

Channel 12 News kimeviweka vyama vya Blue and White na cha Likud kujinyakulia viti 32 kila mmoja huku matokeo yaliobadilishwa ya Channel 13 News yakitabiri kuwa chama cha Blue and White kitashinda viti 33 huku cha Likud kikijinyakulia 31.

Kulikuwa na ukimya katika makao makuu ya chama cha Likud mjini Tel Aviv wakati matokeo hayo yakitangazwa ya baada ya kufungwa vituo vya kupiga kura.