Ofisa wa magereza ajiua mahakamani

Muktasari:

Ofisa wa magereza nchini Ruusia amejiua akiwa ameshahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kutokana na kujipatia fedha kinguvu

Ofisa wa juu wa zamani wa magereza nchini Russia amejiua kwa kujipiga risasi akiwa mahakamani jijini Moscow baada ya kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kujipatia fedha kinguvu, amesema msemaji wa mahakama.
Viktor Sviridov, ambaye awali alikuwa kiongozi wa idara ya usafiri ya magereza,
"alijiua akiwa ndani ya chumba cha mahakama kwa kujipiga risasi kifuani," msemaji huyo wa mahakama ya jiji la Moscow aliiambia AFP.
Hakutoa maelezo zaidi ya tukio hilo.
Bastola ambayo Sviridov aliitumia alipewa kama zawadi, mwanasheria wake Alexander
Kotelnitsky alikiambia kituo cha televisheni cha 24.
Sviridov alishakiri makosa ya kupora dola 159,000 (sawa na zaidi ya Sh3000
milioni) kutoka kwa naibu wa zamani wa magereza. Mahakama hiyo ilimuhukumu kifungo
cha miaka mitatu jela.
Hukumu yake ilikuwa chini ya kiwango cha juu cha hukumu ya miaka 15 aliyostahili
kupewa kutokana na kubainika kuwa na ugonjwa wa saratani, vyombo vya habari vya Russia viliripoti.
Haikueleweka ofisa huyo wa zamani, ambaye amekuwa akishi nyumbani kwake tu kutokana na kuzuiwa kusafiri, alimudu vipi kuingia mahakamani na bastola wakati mlangoni kuna vifaa vya kung'amua vitu vya chuma.
Msemaji wa Mahakama ya Jiji la Moscow alisema wapelelezi wanachunguza mazingira ya kuingia kwake.
Wanaochunguza rushwa katika magereza ya Russia wameanika ukiukwaji mkubwa wa taratibu unaohusisha  maofisa na tayari baadhi wamejiua.
Kiongozi wa zamani wa magereza, Alexander Reimer, alihukumiwa miaka nane jela mwaka 2017 kwa kosa la kuiba mamilioni ya fedha za serikali zilizotengwa kununua vifaa vya kielektroniki.