Polisi Ethiopia yaomba radhi kutangaza kifo cha mlinzi wa mkuu wa majeshi

Muktasari:

  • Mlinzi huyo anadaiwa kumfyatulia risasi Jenerali Seare Mekonen Jumamosi iliyopita alipokuwa akizuia jaribio la mapinduzi lililotokea katika Serikali ya Amhara

Ethiopia. Jeshi la Polisi nchini Ethiopia limeomba radhi kwa madai ya kutangaza kifo cha mlinzi wa Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Seare Mekonnen baada ya kujiua mwenyewe kwa risasi.

Mlinzi huyo anadaiwa kumfyatulia risasi Jenerali Mekonen Jumamosi jioni June 22, alipokuwa akizuia jaribio la mapinduzi lililotokea katika Serikali ya Amhara.

Pia, katika jaribio hilo kiongozi wa Serikali hiyo, Ambachew Mekonnen na mshauri wake, Ezez Wasie wameuawa baada ya kuvamiwa katika ofisi zao eneo la Bahir Dar na kikundi cha wanajeshi wanaodaiwa walidhamiria kufanya mapinduzi.

Kufuatia tukio hilo polisi nchini humo jana asubuhi walisema kuwa mlinzi huyo amefariki dunia baada ya kujifyatuli risasi.

Hata hivyo, taarifa ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari baadaye jioni ilisema mlinzi huyo kwa sasa yupo hospitalini akipatiwa matibabu. Hata hivyo, taarifa hiyo haikutaja hospitali gani.

Kwa mujibu wa ofisi ya Waziri Mkuu, mlinzi huyo anatuhumiwa kuwaua jenerali Seare na msaidizi wake Jenerali Gezai Abera waliokuwa katika ofisi yao siku ya Jumamosi ikiwa ni sehemu ya jaribio la mapinduzi katika Serikali ya Amhara.

Hii ni mara ya pili taarifa ya mlinzi huyo kubadilika. Awali mara baada ya tukio hilo Serikali ilisema inamshikilia mlinzi huyo kabla ya Mkuu wa polisi nchini humo, Endeshaw Tasew kutangaza kifo chake jana baada ya kujiua mwenyewe.