Polisi wakiri makosa kumdhibiti Bobi Wine

Kampala (Daily Monitor). Polisi nchini Uganda wamekiri kufanya makosa kisheria katika kudhibiti mikutano ya ndani ya mwanasiasa machachari, Robert Kyagulanyi.

Mbunge huyo wa Kyadondo Mashariki  maarufu kama Bobi Wine amekuwa akiandaa mikutano ya mashauriano na maoni katika wilaya mbalimbali kuhusu azima yake ya kuwaniwa urais, lakini mara zote wameingilia kati na kuvunja mikutano hiyo, licha ya kuruhusiwa na Tume ya Uchaguzi (EC).

Vilevile, Bobi Wine naye alikiri kuwa yeye na kundi lake pia wamefanya baadhi ya makosa kwa kutofuata ushauri wa EC wa kutaka wasiwe na maandamano wakati wa mikutano hiyo.

Hayo yamefikiwa katika kikao walichofanya na maofisa wa EC Kampala jana, kati ya polisi, Bobi Wine na wagombea wengine watatu wa urais.

Kikao hicho kilifanyika huku polisi wa Kikosi cha kutuliza ghasia wakiwa wamezingira eneo la Tume hiyo ili kudhibiti wafuasi wa mbunge huyo.

Desemba 20, EC ilimruhusu Bobi Wine na wengine watatu kwenda katika maeneo mbalimbali nchini kuchukua maoni ya umma kuhusu nia yao hiyo.

Wagombea wengine ni John Nkugabwa, Fred Mwesigye na Joseph Mwambazi.

Lakini Januari 6 pale Bobi Wine alipotaka kufanya mkutano wa kwanza katika eneo la Gayaza jimboni kwake polisi walizingira eneo na kukatokea makabiliano na wafuasi wa mbunge huyo.

Pia mji wa Kasangati ulifunikwa na moshi wa mabomu na milio ya risasi wakati polisi wakikabiliana na wafuasi wa Bobi Wine.

Mbunge huyo, watu wengine wa kundi la People Power na wafuasi wake walikamatwa na polisi kabla ya kuachiwa baadaye.