Polisi watawanya mkutano wa wafuasi wa Ruto

Mumias. Polisi nchini Kenya wametumia mabomu ya machozi kuwazuia wafuasi wa Naibu Rais, William Ruto kufanya mkutano sambamba na ule wa Jopo la Maridhiano (BBI) katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega.

Matukio ya polisi wakikabiliana na wafuasi wa Ruto yameshuhudiwa katika maeneo ya Ekero na Shibale mjini Mumias, Kaunti ya Kakamega ambapo walirusha mabomu ya kutoa machozi na kuzima juhudi za viongozi wao kuhutubia dhidi ya BBI.

Mkutano wao wa Nabongo ulifutwa na vyombo vya usalama.

Makabiliano hayo yalishuhudiwa dakika chache baada ya viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa na Seneta wa zamani wa Kaunti ya Kakamega, Dk Boni Khalwale kushutumu maofisa wa polisi kuhusu kutoweka kwa Ben Washiali, mbunge wa Mumias Mashariki ambaye alitarajiwa kuwaongoza.

Maofisa wa polisi walitawanya umati uliokuwa eneo la Ekero, ukihutubiwa na Echesa.

Viongozi wengine waliokuwepo ni wabunge Justus Murunga (Matungu), John Walukhe (Sirisia), Didmus Barasa (Kiminini), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), na Charles Gimose (Hamisi).

Hali hiyo imelazimu hadhira kutawanyika na viongozi hao waondoka na kuelekea Shibale ambako pia maofisa waliwakabili.

Katika daraja la Mto Nzoia lililopo baina ya Ekero na Shibale, polisi walilazimika kuzima moto uliowashwa katikati ya barabara ya Mumias-Bungoma na wafuasi wa kundi hilo.

Viongozi hao wamesema wataandaa mkutano wao mwishoni mwa wiki ijayo.

Mbunge Murunga alisema walikuwa wamenuia kutumia mkutano wao huo mbadala kudhihirisha wao si waoga.

Jopo la Maridhiano lilitoa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ya Kenya yenye lengo la kumaliza mpasuko wa kisiasa na linaendelea kuyafafanua kwa umma, likipingwa na kundi la wanasiasa linaloaminika kuwa nyuma ya Ruto.