Polisi wazingira nyumba ya Bobi Wine, wamzuia kushiriki tamasha

Wednesday October 9 2019

 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi [email protected]

Uganda. Leo Jumatano Oktoba 9, 2019 Jeshi la Polisi nchini Uganda limeizunguka nyumba ya Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine kwa lengo la kumzuia asishiriki tamasha mjini Kampala.

Tamasha hilo la Osobola lilipangwa kufanyika kwenye ufukwe wa One Love unaomilikiwa na Bobi Wine uliopo eneo Busabala jijini humo.

Askari wameweka uzio katika njia mbili zinazotumika kufika nyumbani kwa Boni Wine ambaye pia ni msanii wa muziki   na kuweka kizuizi cha vyuma chenye ncha kali na kukagua kila gari linalotoka na kuingia.

Mmoja wa majirani wamesema waliona polisi wakizingira nyumba hiyo kuanzia jana usiku Jumanne Oktoba 8, 2019.

“Nilipokuwa nakuja nyumbani jana usiku nilikuta polisi wamefunga njia na wanisimamisha. Niliwaeleza naelekea nyumbani kwangu hapo ndipo waliniachia,” amesema Dennis Kamoga.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter,  Bobi Wine amesema tangu saa 11 alfajiri polisi wamezunguka nyumba yake na eneo la fukwe, “wananiweka chini ya ulinzi kwenye nyumba yangu na kuzuia tamasha la muziki la siku ya uhuru.”

Advertisement

“Kwa kuimba ukweli kwa viongozi, siwezi kufanya onesho kwenye nchi yangu.”

Leo ni siku ya uhuru wa Uganda  na jana polisi walitoa taarifa ya kusitishwa tamasha hilo kwa sababu za kiusalama.

Hata hivyo,  Bobi Wine amesema tamasha hilo litafanyika kama lilivyopangwa huku msemaji wa polisi, Patrick Onyango akiwataka wananchi kutokwenda katika tamasha hilo.

“Kama unataka amani kaa nyumbani kwenu kwa sababu hakuna tamasha kesho (leo). Usipoteze muda wako tafadhali” amesema Onyango.

Advertisement