Raia wa Korea Kusini, Italia hatarini kuzuiwa Marekani kutokana na corona

Muktasari:

  • Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kutokana na maambukizi wa virusi vya corona nchi hiyo inachukua tahadhari  mapema.

Washington. Korea Kusini na Italia huenda zitaongezeka katika nchi ambazo raia wake wanazuiwa kuingia Marekani kufuatia maambukizi ya virusi ya corona kuwa ya kasi sana katika nchi hizo.

Hadi sasa Korea Kusini kuna waathirika 1,595 na Italia zaidi ya 400 na watu 12 wamekufa katika nchi hizo.

“Kuhusu Korea Kusini muda ukifika tutafanya hivyo, kwa sasa muda bado na Italia tatizo linazidi kuwa kubwa tunawakagua kila wakiingia kwa umakini wa juu ila itafika hatua tutasitisha,” amesema Rais Donald Trump.

Trump amesema kusambaa kwa virusi hivyo ni jambo lisilozuilika na amemteua Makamu wa Rais, Mike Pence kuwa kiongozi wa mapambano ya ugonjwa huo.

“Nafikiri ni kitu kisichozuilika, kuna uwezekano suala hili likawa baya zaidi,” amesema Trump.

Vituo vya kupambana na kuzuia magonjwa Marekani imetoa onyo kwa wananchi kujiandaa kuahirisha kufika sehemu zenye mikusanyiko.

 

Tayari raia kutoka China wamezuiwa kuingia Marekani huku nchi hiyo ikisema ongezeko la baadhi ya nchi zenye maambukizi hayo zitaongezeka.

China hadi sasa waliokufa ni 2,744 na kufikia leo Februari 27 nchi ambazo zimepata wagonjwa wapya ni pamoja na Brazil, Ugiriki, Norway na Pakistan ikiashiria ugonjwa unazidi kuenea duniani na Afrika ni nchi mbili zilizopata wagonjwa nazo ni Misri na Algeria.

Maambukizi ya virusi vya corona yalianza mwaka jana nchini China na hadi sasa yameenea nchi mbalimbali duniani na waathirika wakifikia 80,000 na waliokufa ni zaidi ya 2,700. Shirika la Afya Duniani (WHO) imeitahadharisha dunia kujiandaa kwa ugonjwa huo ukiutaja kama ni janga.