Rais Bolivia ajiuzulu baada shinikizo la maandamano

Rais wa Bolivia aliyejiuzulu, Evo Morales

Sucre. Rais wa Bolivia, Evo Morales amelazimika kujiuzulu  baada ya kukosa uungaji mkono wa Jeshi na polisi, kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi uliompa ushindi Oktoba 20 mwaka huu.
Jana Jumapili,  Rais huyo alikuwa ametangaza uchaguzi mpya baada ya wiki kadhaa za maandamano dhidi ya madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa rais, lakini Mkuu wa Majeshi alimjibu kwamba yeye ndio ajiuzulu kwa usalama wa Bolivia.
Baada ya kujiuzulu, Rais huyo amedai kwa sasa kuna hati ya kumkamata, madai ambayo vyombo vya usalama vimeyakanusha.
“Ninaitangazia dunia na watu wa Bolvia kwamba ofisa wa polisi amesema waziwazi kuwa amepewa maelekezo ya kutekeleza amru isiyo halali ya kunikamata,” Morales aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.
Lakini Kamanda wa Polisi, Vladimir Yuri Calderon aliieleza televisheni moja ya Bolivia kuwa hakuna hati kama hiyo.
Morales amesema vikundi vya vurugu vimevamia nyumbani kwake na kuwa “wahaini wanaharibu utawala wa sheria”.
Kiongozi wa maandamano hayo ya wiki tatu yaliyopelekea Morales kujiuzulu, Luis Fernando Camacho, amesema kulikuwa na agizo la kumkamata rais huyo mstaafu.
Alisema jeshi limechukua ndege ya Rais na kuwa yeye (Morales) amejificha huko Chapare ambako wanamfuata.
Morales alitangaza kujiuzulu kwake kupitia televisheni akiwa huko Chapare.
Atangaza kurudia uchaguzi
Mapema akitangaza kurejea uchaguzi, Rais huyo alisema ameamua kuitisha uchaguzi mpya ili wananchi wa Bolivia waweze kuchagua serikali mpya kwa njia ya kidemokrasia.
Kwa wiki kadhaa Bolivia imeshuhudia machafuko na ghasia dhidi ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa Oktoba 20.
Watu watatu wameuawa na zaidi ya 300 kujeruhiwa katika vurugu hizo za kupinga udanganyifu katika uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi uliopita yalimpa ushindi Morales kwa asilimia 10 zaidi ya mpinzani wake, Carlos Mesa.
Upande wa upinzani umekuwa unaishutumu serikali kwa udanganyifu.