Rais Fifa ashangaa kukuta uwanja mtupu Korea Kaskazini

Muktasari:

  • Infantino alikuwa ameenda kushuhudia mechi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia la soka baina ya Korea Kusini na Kaskazini iliyofanyika jana jijini Pyongyang.

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Gianni Infantino amesema 'alikerwa" kuhudhuria mechi ya kihistoria ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia baina ya Korea Kusini na Kaskazini iliyochezwa kwenye uwanja mtupu na ambayo haikurushwa moja kwa moja na televisheni.
Mechi hiyo ya nadra kufanyika Korea Kaskazini iliisha kwa sare ya bila kufungana jana Jumanne, Infantino akiwa mmoja wa watu wachache walioruhusiwa kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kim Il ulio jijini Pyongyang.
"Nilikuwa natarajia kuona uwanja umejaa katika mechi kama hii ya kihistoria, lakini niliudhika kuona hakukuwa na mashabiki jukwaani," alisema katika mahojiano yaliyochapishwa na tovuti ya Fifa.
"Tulishangazwa na hili na mengine kadhaa yanayohusu matangazo ya moja kwa moja na matatizo ya visa na ruhusa kwa waandishi wa habari kutoka nje ya nchi."
Hakuna vyombo vya habari vilivyoruhusiwa kwenye mechi hiyo -- ambayo ni ya kwanza ya mashindano baina ya nchi hizo kuchezwa Pyongyang. Kiufundi nchi hizo mbili bado ziko vitani.
Mashabiki wa Korea Kusini waliochanganyikiwa kwa kutoruhusiwa kusafiri kwenda kuona mechi hiyo, watalazimika kusubiri siku kadhaa kuiona kwenye televisheni baada ya viongozi wa timu watakaporudi na DVD ya mchezo huo.
"Kwetu, uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza ni vitu muhimu, lakini kwa upande mwingine itakuwa ni ujinga kudhani kuwa tutaweza kuibadili dunia kuanzia dakika moja hadi nyingine," alisema Infantino.
Mechi hiyo imekuja wakati Korea Kaskazini ikifanya mfululizo wa majaribio ya makombora yake na kuzua taharuki kwenye eneo hilo, na baada ya kuvunjika kwa mazungumzo na Marekani kuhusu silaha za Korea Kaskazini.