Rais Mubarak kuzikwa leo

Muktasari:

Rais Hosni Mubarak aliyetawala Misri kwa miaka 30, atazikwa kesho Jumatano kwa heshma za kijeshi.

Cairo, Misri. Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubaraka anatarajiwa kuzikwa leo.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la AFP, Rais huyo aliyefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 91 atazikwa kwa heshima za kijeshi.

Jumamosi iliyopita mtoto wa kiume wa kiongozi huyo, Alaa Mubarak aliandika katika ukurusa wake wa mtandao wa Twitter kuwa baba yake alikuwa akipatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Mtoto huyo alisema baba yake alifanyiwa upasuaji mwezi Januari lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

Viongozi mbali mbali wa dunia wametoa salamu zao za rambirambi wakisifu mchango wake alioutoa katika kusimamia nchi hiyo iliyopo Mashariki ya Kati.

Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas alisema Mubarak alipigania haki za Wapalestina.

 

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyau alisema  kiongozi huyo alihakikisha anasimamia amani na usalama wa watu wake na kukamilisha amani na Israel.

Ayman Nouur, mpinzani wa muda mrefu Misri na mgombea urais ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Uturuki alisema amemsamehe kiongozi huyo.