Rais Nigeria aonya waandamanaji

Muktasari:

Rais wa Nigeria ameshauri kumalizwa kwa vurugu zinazosambaa nchi yote, lakini akakwepa kutaja kitendo cha polisi wa Lagos kufyatulia risasi waandamanaji wasio na silaha ambacho kimesababisha jumuiya ya kimataifa ikilaani na kuzidisha vurugu katika jiji hilo kubwa kuliko yote barani Afrika.

Lagos, Nigeria . Rais wa Nigeria ameshauri kumalizwa kwa vurugu zinazosambaa nchi yote, lakini akakwepa kutaja kitendo cha polisi wa Lagos kufyatulia risasi waandamanaji wasio na silaha ambacho kimesababisha jumuiya ya kimataifa ikilaani na kuzidisha vurugu katika jiji hilo kubwa kuliko yote barani Afrika.

Lagos imeshuhudia ufyatuaji wa risasi, maduka kuvamiwa na magereza kuchomwa moto tangu vikosi vya usalama vilipowafuatulia risasi watu waliokuwa wakiandamana kwa amani, wakitaka utawala bora na kupinga ukatili wa polisi katika jiji hilo lenye watu milioni 20.

Taasisi ya haki za binadamu ya Amnesty International ilisema wanajeshi wa Nigeria na polisi waliwaua kwa risasi waandamanaji 12, wakati kwa ujumla watu 56 wamefariki nchini kote tangu maandamano yalipoanza wikimbili zilizopita.

Jana Alhamisi, Rais Muhammadu Buhari alionya waandamanaji kutopuuza "usalama wa taifa" katika hotuba yake ya kwanza tangu tukio hilo la Jumanne, ambalo alikwepa kulitaja moja kwa moja.

Badala yake, alilaumu wachochezi ambao alisema wameteka na kupotosha" malengo ya waandamanaji.

"Katika mazingira yoyote hili haliwezi kuvumiliwa," alisema Buhari.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 77 aliwataka vijana "kuacha maandamano mitaani na kuishirikisha serikali kutafuta suluhisho".

Matamko ya kulaani tukio hilo duniani yamekuwa yakiongezeka, huku Marekani, Umoja wa Afrika na Uingereza, zikilaumu mamlaka kwa kutumia nguvu kupita kiasi.