Rais Omar al Bashir ahukumiwa miaka miwili

Rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir

Muktasari:

Kwa mujibu wa sheria za Sudan kuanzia miaka 70 anasamehewa kwenda jela hivyo Rais huyo wa zamani atakwenda katika kituo cha kijamii kwa miaka miwili.

Khartoum, Sudan. Rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir amehukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kituo cha kijamii baada ya kupatikana na kosa la ufisadi.

Kiongozi huyo aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 30 alihukumiwa leo Jumamosi Desemba 14.

Kwa mujibu wa sheria za Sudan watu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 hawahutumikii kifungo cha jela hivyo kongozi huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 75 atapelekwa katika kituo cha jamii.

Bashir alikuwa akikabiliwa na kesi ya ufisadi ambako alidaiwa kuficha fedha za kigeni zenye thamani ya dola milioni 25, zilizopatikana katika nyumba yake muda mfupi baada kung'olewa madarakani mwezi Aprili, mwaka huu.

Hata hivyo, pamoja na hukumu hiyo, Rais Bashir bado anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Muda mfupi kabla ya kusomwa kwa hukumu dhidi yake, baadhi ya wafuasi wa Rais huyo wa zamani walianza kushangilia kwa sauti ya juu wakisema kesi ilikuwa ni ya kisiasa kabla ya hakimu kuwaamuru watoke nje ya mahakama.

Katika mashtaka hayo, Bashir anadaiwa kupokea kiasi hicho cha fedha za nje kutoka kwa Mwanamfalme wa Saudia Arabia, Mohammed bin Salman.

Katika utetezi wake, Rais Bashir aliieleza Mahakama kwamba malipo hayo yalifanyika kama sehemu ya mkakati wa Sudan wa uhusiano na Saudi Arabia na hazikutumiwa kwa maslahi binafsi.

Baada ya hukumu kutolewa mmoja wa mawakili wa kiongozi huyo, Ahmed Ibrahim aliliambia Shirika la habari la Ufaransa (AFP), kwamba mteja wake amepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Mohamed al-Hassan, wakili mwingine wa Bashir, alisema kuwa upande wa utetezi haukuichukulia kesi hiyo kwa mujibu wa sheria na badala yake walifanya siasa zaidi.