Rais Ramaphosa aiomba radhi Nigeria kuhusu ubaguzi wa wageni Afrika Kusini

Muktasari:

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameiomba radhi Nigeria kutokana na ubaguzi dhidi ya wageni ulioibuka nchini humo, huku raia wa mataifa hayo mawili wakiingia katika mzozo.
Mwandishi Wetu, Mwananchi

Abuja. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameiomba radhi Nigeria kutokana na ubaguzi dhidi ya wageni ulioibuka nchini humo, huku raia wa mataifa hayo mawili wakiingia katika mzozo.
Katika vurugu hizo zilizoibuka mwanzoni mwa Septemba 2019 watu 12 waliuawa baada ya raia wa Afrika Kusini kushambulia biashara za wageni, hasa mjini Johannesburg.
Rais Ramaphosa alituma mjumbe maalum kuomba radhi kwa Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari.
Mjumbe huyo, Jeff Radebe aliwasilisha ujumbe huo katika mkutano maalumu baina yake na Buhari uliofanyika katika mji mkuu Nigeria, Abuja leo Jumanne Septemba 17, 2019.
“Tukio hilo haliwakilishi tunachosimamia. Polisi wa Afrika Kusini hawataacha kuwachukulia hatua waliohusika katika tukio hilo,” ameeleza mjumbe huyo.
Amemueleza Buhari kuwa Afrika Kusini inalaani vurugu hizo na tayari imeshaanza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika wote.
Rais Buhari alimshukuru mjumbe huyo kwa kutoa ufafanuzi kuhusu ubaguzi huo uliosababisha mauaji ya raia wa kigeni, kuridhia msamaha wa Ramaphosa na kuahidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuendelezwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Ramaphosa alilieleza Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kuwa anaona aibu kwa vurugu hizo.
Wakati hayo yakiendelea,  Afrika Kusini imefunga balozi zake mjini Lagos na Abuja  kutokana na vurugu zinazowalenga maofisa wa balozi hizo ikiwa ni kulipa kisasi kwa mashambulizi ya wageni Afrika Kusini.