Rais Trump afuta ziara ya Denmark

Muktasari:

  • Rais Dornald Trump amefuta ziara hiyo kufuatia uamuzi wa Waziri mkuu wa Denmark kutatangaza kuwa Serikali yake haipo tayari kuiuzia Marekani kisiwa cha Greenland.

Washington, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kufuta ziara yake ya nchini Denmark iliyopangwa kufanyika baada ya wiki mbili.

Shirika la habari la BBC lilisema kuwa Rais Trump amefuta ziara hiyo kufuatia uamuzi wa Waziri Mkuu wa Denmark kutatangaza kwamba nchi yake haiko tayari kukiuza kisiwa chake cha Greenland kwa Marekani.

Awali Rais Trump alitarajiwa kuzuru Taifa hilo Septemba 2, kufuatia mwaliko wa malkia Margrethe II.

Mapema wiki iliopita Rais Trump alitangza kwamba Marekani ilikuwa na nia ya kukinunua kisiwa kinachojitawala cha Greenland kilichopo katika Jimbo la Denmark.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen alitaja mpango huo wa Marekani ni kipuuzi na kusema kwamba anaamini Rais Trump hakulichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, Rais Trump alisema “Denmark ni Taifa maalum lenye watu wazuri lakini kutokana na matamshi ya Waziri mkuu Mette Frederiksen kwamba hatakuwa na hamu ya kuzumngumzia ununuzi wa Greenland nitaahirisha mkutano wangu uliopangwa wiki mbili zijazo kwa muda mwengine.”

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, alithibitisha kufutwa kwa ziara hiyo.