Rais Trump akalia kuti kavu, mchakato wa kumng’oa madarakani waanza

Muktasari:

  • Ni baada ya Spika wa Bunge la Marekani, kutangaza mchakato wa kumng’oa madarakani.

Washington, Marekani. Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi ametangaza kuanzisha mchakato wa kumng’oa madarakani Rais Donald Trump.

Tamko la Spika Nancy ambalo amelitoa jana Jumanne Septemba 24 ni hatua ya kwanza katika mchakato ambao unaweza kumuondoa Rais huyo madarakani.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la AFP, hatua ya Spika Nancy inafuatia madai kuwa Julai 25 Trump alizungumza kwa simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kutaka msaada wa kumuangamiza mpinzani wake katika kampeni yake ijayo ya uchaguzi.

Aidha, katika mazungumzo hayo Trump inadaiwa alimshinikiza Rais wa Ukraine kutafuta njia za kuchafua sifa ya makamu wa Rais wa zamani, Joe Biden na mtoto wake, Hunter. Kupitia tiketi ya chama cha Democratic, Biden anaweza kuwa mpinzani wa Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa 2020.

Lakini jana Spika Nancy alisema “inasikitisha sana kufikiria kwamba Rais wetu anaweza kufanya kosa la kufunguliwa mashtaka. Ni ngumu unajua? Ni ngumu kusema tumefika katika hali hiyo,” alisisitiza Spika Pelosi akitoa taarifa hiyo kwa njia ya televisheni.

Kupitia tangazo lake Spika Nacy alisema uchunguzi maalumu utafanywa ili kubaini ukweli kisha kura zitapigwa na wabunge kupata fursa ya kuamua.

Spika Pelosi aliongeza kuwa kamati nyingine sita zinazofanya uchunguzi wa masuala mengine dhidi ya Trump zitaendelea na kazi yao chini ya uchunguzi wa sasa.

Rais Trump yuko katika wakati mgumu kutokana na hoja hiyo kuungwa mkono na wafuasia wa Chama cha Democrats juu ya uchunguzi huo ambao unaoweza kumuondoa madarakani.

Ikiwa uchunguzi huu utaendelea, Bunge la wawakilishi litapigia kura mashtaka yoyote yatakayobainika na kwa kwa kuwa chama cha Democrats ndio kina wawakilishi wengi katika Bunge hilo la congress kinaweza kupitisha umuzi mgumu dhidi ya kiongozi huyo.

Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa iwapo mchakato huo utaendelea huenda usipitishwe na Baraza la Seneti ambalo linawajumbe wengi kutoka Chama cha Republicans na kwa mujibu wa sheria inahitajika theluthi tatu ya kura za wabunge hivyo ni rahisi kwao kuzuia mchakato huo.

Mchakato wa kumng’oa Rais Trump umechochewa na ripoti za jasusi aliyefichua malalamiko kuhusu simu ambazo kiongozi huyo alimpigia mwenzake wa Ukrain rais Volodymyr Zelensky.

Kwa upande wake Trump amekanusha vikali madai hayo na kudai kuwa mazungumzo yalikuwa ya kirafiki huku akizitaja juhudi za kumtuhumu kama hila chafu dhidi yake.

Rais Trump akiri kuzungumza na viongozi hao lakini akasema alikuwa tu akijaribu kuitaka Ulaya iingilie kati kutoa msaada kwa kuitishia kusitisha msaada wa kijeshi.

Trump pia alikiri kwamba kwa muda mfupi alizuia fedha za msaada kwa Ukraine kiasi cha dola milioni 400 si kwa lengo la la kumshinikiza Zelenskiy aanzishe uchunguzi ambao utaharibu sifa ya Biden. Pesa hizo za misaada hatimaye zilitolewa wiki iliyopita.