Rais wa zamani Marekani alazwa hospitali

Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter

Muktasari:

Ni Jimmy Carter ambaye amelazwa kutokana na tatizo la ubongo baada ya kuanguka.

Washington, Marekani. Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter amelazwa hospitalini baada ya kugundulika kuwa na tatizo katika ubongo wake.

Kiongozi huyo wa zamani  aliyeongoza Marekani kuanzia mwaka  1977 hadi 1981 amelazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Emory jana Jumatatu Novemba 11.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Ufaransa (AFP), Rais huyo mwenye umri wa miaka 95 alipata tatizo hilo baada ya kuanguka mwezi Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa siku moja baada ya tukio hilo kiongozi huyo alionekana katika hadharani akiwa amejeruhiwa jicho na kufungwa bandeji.

Inadaiwa kuwa katika tukio hilo kiongozi huyo aliumia kichwani na kusababisha damu kutoka na kuathiri ubongo. Hata hivyo, haikuelezwa zaidi hali ya kiongozi huyo kwa sasa inaendeaje.

Taarifa ya hospitali hiyo kwa vyombo vya habari ilisema kuwa “Rais Carter amepumzika vizuri na mkewe, Rosalynn yuko naye pembeni.”