Breaking News

Saad al-Hariri: Sihitaji uwaziri mkuu tena

Wednesday November 27 2019

 

Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad al-Hariri amesema kuwa hataki tena wadhifa huo katika Serikali mpya.

Kiongozi huyo ambaye alitangaza kujiuzulu hivi karibuni alisema uamuzi wake ni wa kweli, muhimu na kwamba ana imani na Rais Michel Aoun.

“Naomba wateue mtu mwingine,” alisema Hariri kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Alisema kwa sasa anahitaji kupumzika ili kupisha watu wengine kuiongoza nchi hiyo na kwamba uamuzi wake ni lazima uheshimiwe.

Alisema Walebanon wanapaswa kuteua mtu mwingine atakayeunda Serikali itakayoshughulikia matakwa ya vijana na wanawake.

Alisema ana imani baada ya kutangaza uamuzi wake huo, Rais ataitisha kikao cha Bunge cha ushauri ili kumpata waziri mkuu mpya.

Advertisement

Saad al-Hariri alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu baada ya maandamano makubwa ya wiki kadhaa ambako vijana walifunga barabara na kushinikiza kuondoka madarakani kwa Serikali yote kutokana na ukosefu wa ajira na ughali wa maisha.

Mapema mwezi huu, vyama vikuu vitatu nchini humo vilikubaliana kumteua Mohammad Safadi

Safadi aliyewahi kuwa waziri wa zamani wa fedha, ameteuliwa kuwania nafasi hiyo kuwa waziri mkuu katika hatua ya kuelekea kuundwa Serikali mpya katika wakati ambao kuna mgogoro mkali wa kiuchumi.

Makubaliano ya kumteuwa Safadi yameafikiwa katika mkutano kati ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Saad al-Hariri, ambaye ni mwanasiasa mashuhuri wa madhehebu ya Sunni anayeegemea mataifa ya Magharibi na ya Ghuba na wawakilishi wa kundi la madhehebu ya Shia la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran na mshirika wake wa Kishia Amal.

Habari hizo ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari vya Lebanon.

Hariri alijiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu Oktoba 29, kutokana na wimbi kubwa la maandamano dhidi ya watawala wa kisiasa wanaolaumiwa kwa kukithiri ufisadi serikalini na kuitumbukiza Lebanon katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1975 hadi 1990

Advertisement