Saudi Arabia yazuia wageni kutembelea miji ya Makka, Madina

Muktasari:

Serikali ya Saudi Arabia imezuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini ikiwemo wanaotembelea miji mitakatifu katika dini ya Kiislamu ya Makka na Madina kutokana na tishio la virusi vya corona (Covid-19).

Riyadh. Serikali ya Saudi Arabia imezuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini ikiwemo wanaotembelea miji mitakatifu katika dini ya Kiislamu ya Makka na Madina kutokana na tishio la virusi vya corona (Covid-19).

Mamilioni ya watu huingia Saudi Arabia mwaka mzima kufanya ibada ya Umra (ibada kipindi ambacho siyo cha hija) na wengi zaidi huingia kwa pamoja kufanya ibada ya Hija.

Mbali na Hija, watu wengi hutembelea miji hiyo na Umra hufanyika katika kipindi chote cha mwaka na kwa sasa marufuku hiyo inawalenga mahujaji raia wa nchi za nje wanaoenda kuitekeleza.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, bado haijulikani kama ibada ya Hija ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa Julai kama itaathirika na zuio hilo pamoja na kusambaa kwa virusi vya corona duniani.

Saudia pia imewapiga marufuku watu kutoka nchi zilizokumbwa na virusi hivyo kuingia nchini humo. Mpaka sasa Saudi Arabia bado haina mtu ambaye amethibitika kuambukizwa virusi hivyo.

Makka ndiyo mji ambao Mtume Muhammad alizaliwa na kuna msikiti maalumu wakati Madina ndiyo mahali alipofariki na kuzikwa. Miji hiyo imebeba historia kubwa katika imani ya dini ya Kiislamu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imesema marufuku hiyo ni ya muda, hata hivyo, wizara hiyo haijataja lini marufuku hiyo itaondolewa.

Watalii ambao siyo wa kidini ambao wanatoka katika nchi ambazo virusi vya corona vimethibitishwa kuingia pia watakataliwa kuingia nchini humo. Serikali imebainisha kwamba tangu Oktoba 2019, imetoa viza zaidi ya 400,000 za watalii kutoka nchi mbali mbali duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) mapema wiki hii limeonya kuwa mataifa yanapaswa kujiandaa kwa uwezekano wa janga la virusi vya corona.

Hata hivyo, shirika hilo limesita kuuita mlipuko wa virusi hivyo janga lakini lakini imetoa wito kwa nchi kuwa katika “awamu ya maandalizi”. WHO ilifafanua kwamba janga ni pale maambukizi ya ugonjwa yanaposambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine katika maeneo mengi ya dunia.

Visa zaidi vya virusi ambavyo husababisha ugonjwa kupumua Covid-19, vinaendela kujitokeza, huku milipuko ya ugonjwa huo vikibainika katika mataifa mengi zaidi nje ya China ambako ndiyo ulianzia.

Mpaka sasa zaidi ya watu 2,700 wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 wakati zaidi ya watu 80,000 duniani kutoka katika mataifa 40 wakiambukizwa virusi hivyo, wengi wao wakiwa China.

Iran ambayo inapakana na Saudi Arabia, mpaka sasa imeripoti vifo 19 ambayo ni idadi kubwa zaidi ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo nje ya China.