Breaking News

Serikali Urusi yajiuzulu

Wednesday January 15 2020

 

Moscow, Urusi. Waziri mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev ametangaza kujiuzulu akisema kuwa yeye pamoja na serikali anayoiongoza inaachia ngazi ili kumpa nafasi Rais Vladmir Putin kufanya mabadiliko ya Katiba

Medvedev aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Putin jana jioni kisha kutoa tamko hilo kupitia Televisheni ya Taifa ya Urusi akiwa ameketi sambamba na Rais Putin ambaye ni mshirika wake wa karibu.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Urusi, Putin amemshukuru waziri mkuu huyo aliyejiuzulu kwa utumishi wake huku akibainisha kuwa baraza lake la mawaziri lilishindwa kutimiza majukumu yake.

Medvedev ametumikia wadhifa huo wa uwaziri mkuu wa Urusi tangu mwaka 2012, kabla ya hapo alikuwa Rais wa nchi hiyo toka mwaka 2008 hadi 2012.

Baada ya kujiuzulu kwa Medvedev na mawaziri wake Rais Putin ameliomba baraza hilo la mawaziri kuendelea kufanya kazi hadi litakapotangazwa lingine.

Tangazo la waziri mkuu huyo ambalo halikutarajiwa  limetolewa muda mfupi baada ya Rais Putin  kutoa hotuba mapema jana jioni akipendekeza kura ya maoni juu ya mabadiliko kadhaa kwenye Katiba ya nchi yake yatakayolipa Bunge nguvu zaidi.

Advertisement

Hatua hiyo huenda ikachochea uvumi juu ya hatma ya Rais Putin baada ya kuwa madarakani kwa miaka 20

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Urusi hajadokeza chochote juu ya mipango yake ya nini kitakachofuata mara tu muhula wake wa uongozi utakapomalizika mwaka 2024.

Aidha, kiongozi huyo alipendekeza mabadiliko ya Katiba katika hotuba yake ya mwaka Ikiwa ni mwaka mmoja pekee uliosalia kuelekea uchaguzi wa Bunge utakaofanyika mwaka 2021 huku chama tawala kikiwa kinakubalika kwa kiwango kidogo.

Baada ya kujiuzulu kwa Medvedev Urusi inahitaji waziri mkuu mpya na baadhi ya wanaotajwa kushika wadhifa huo ni pamoja na Sergei Sobyanin, Meya wa jiji la Moscow, Maxim Oreshkin, waziri wa uchumi au waziri wa nishati, Alexander Novak.

Advertisement