Serikali yapeleka madaktari wa jeshi watoa huduma Zimbabwe

Wednesday September 18 2019

Harare, Zimbabwe. Serikali ya Zimbabwe imepeleka madaktari wa kijeshi katika hospitali za umma ili kutoa huduma baada ya madaktari na wahudumu wa afya nchini humo kugoma.

Mgomo huo wa wafanyakazi wa sekta ya afya ulianza rasmi Septemba 3 nchi nzima na Jumatatu iliyopita kiongozi wa madaktari, Dk Peter Magombeyi alitekwa na watu wasiyo julikana.

Madaktari hao pamoja na mambo mengine wanadai nyongeza ya mshahara kutoka dola 100 za sasa karibu Sh230,000 pamoja na kuboreshewa mazingira ya kazi.

Lakini jana Waziri wa Afya, Obadiah Moyo alisema madaktari wa jeshi watatoa huduma kama hatua ya muda mfupi.

“Hatuwezi kuacha watu wapoteze maisha kwa sababu tu madaktari wamegoma, jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msingi,” alisisitiza waziri Moyo.

Wakati waziri huyo akisema hayo, madakari nchini humo wameendelea kuishinikiza Serikali kusaidia juhudi za kumpata kiongozi wao aliyetekwa nyara.

Advertisement

Inadaiwa kuwa mara ya mwisho kiongozi huyo aliwasiliana na wenzake Jumamosi iliyopita kupitia ujumbe wa WhatsApp akidai alitekwa nyara na wanaume watatu na tangu wakati huo hajaonekana tena na madaktari hao wamesisitiza kuwa hawatarejea kazini mpaka kiongozi wao apatikane.

Mamia ya madaktari katika hospitali za umma nchini Zimbabwe kwa zaidi ya wiki mbili sasa wanafanya mgomo wakishinikiza mishahara yao kulipwa kwa dola ya Marekani ili kukabiliana na gharama za maisha.

Madaktari hao waliliambia Shirika la habari la AFP kwamba wamechoshwa a hali hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

Advertisement