Tetemeko laua 15 Uturuki

Muktasari:

Tukio hilo limetokea jana katika mikoa miwili ya Elazig na Malatya.

Ankara, Uturuki. Watu zaidi ya 15 wamepoteza maisha Mashariki mwa Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Serikali la Anadolu, tetemeko hilo limetokea jana jioni Ijumaa Januari 24.

Shirika hilo lilisema kuwa tetemeko hilo lilitokea kwa nyakati tofauti katika mikoa miwili ya Elazig na Malatya

Aidha, shirika hilo lilisema kuwa katika Mkoa wa Elazig watu 10 waliripotiwa kupoteza maisha na wengine watano mkoani Malatya huku mamia wakijeruhiwa.

Vyombo vya habari nchini humo vilionyesha picha za majengo yaliyoporomoka huku baadhi yakiwa yamefunikwa na kifusi.

Taarifa Shirika la usimamizi wa majanga na dharura nchini humo (AFAD), ilisema kuwa tetemeko hilo lilianzia katika mji wa Sivrice ambao unakabiliwa na matetemeko mara kwa mara.

Awali Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alisema hatua za haraka zimeshaanza kuchukuliwa ili kusaidia watu walioathirika na tetemeko hilo.

Rais Erdogan aliwataka wananchi wa mikoa hiyo kuwa watilivu katika kipindi ambacho Serikali inatafuta ufumbuzi wa janga hilo.