Trump ‘amvaa’ Rais Macron

Muktasari:

Adai 'ubongo uliokufa'

London Uingereza Rais wa Marekani, Donald Trump amemkosoa mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron kutokana na kauli yake kwamba Nato ni ubongo uliokufa.

Rais Trump alisema alichokifanya kiongozi huyo ni matusi na hakipaswi kuvumilika.

Trump alisema hayo nchini Uingereza leo Jumatano Desemba 4 anapohudhuria mkutano wa maadhimisho ya miaka 70 ya Muungano wa kujihami wa mataifa ya Magharibi (Nato).

Rais huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa Nato yenye nchi wanachama 29 inajukumu muhimu.

Awali Rais Macron alisema muungano huo kwa sasa umekufa na unaendeshwa kutokana na utashi wa mdhamini mkuu ambaye ni Marekani.

Mkutano huo ulioanza rasmi leo pamoja na mambo mengine umegubikwa na mzozo mkali miongoni mwa wanachama wake huku suala la namna gani nchi hizo zinachangia umoja huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Trump alisema “amezikosea heshima nchi nyingine wanachama. Matamshi yake ni machafu, nadhani Ufaransa ina kiwango kikubwa cha tatizo la ajira na uchumi wake hauko vizuri.

"Ni matamshi makali sana. Kwanza ni Taifa linalopitia kipindi kigumu hasa ukizingatia kile kinachoendelea. Mwaka huu wamekuwa na wakati mgumu kweli. Huwezi kuanza kuzunguka huku na kule kuisema Nato, huu ukesefu heshima wa hali ya juu,” alisema.

Rais huyo alimshangaa kiongozi huyo na kudai kuwa wakati huu hakuna anayehitaji msaada wa muungano huo kama nchi yake.

“Manufaa inayopata Marekani ni madogo ukilinganisha na mataifa mengine wanachama. Anahitaji ulinzi zaidi ya wengine lakini pia namuona akijiondoa kutoka Nato. Hata hivyo, ni jambo ambalo halijanishangaza."

Naye Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alisema kwamba atapinga mpango wa Nato wa kiulinzi kwa nchi za Baltiki iwapo haitaiunga mkono Uturuki katika vita vyake dhidi ya kikundi cha Kikurdi.