Trump azuia raia wa Ulaya kuingia Marekani

Muktasari:

Ni kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona (covid-19).

Washington, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuweka zuio kwa raia wa nchi za Ulaya kuingia nchini Marekani ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona (covid-19).

Kupitia hotuba yake kwa njia ya televisheni jana Rais Trump alisema safari zote za kutoka Ulaya zitazuiwa kwa siku 30 zijazo.

Trump alikiri nchi hiyo kuchukua hatua kali lakini akasema ni muhimu kwa wakati huu ambako virusi hivyo vinazidi kusambaa kwa kasi duniani.

Wakati kiongozi huyo akitangaza tahadhari hiyo, Wizara ya afya nchini humo imeripoti kuwa na wagonjwa 1,135 ambako 38 kati yao wamepoteza maisha.

Akizungumzia uamuzi huo Trump alisema “Tunaanza kwa kuzuia visa vipya za kuingia Marekani lakini pia tutaahirisha safari zote kutoka Ulaya.

“Hatua hii itaanza kutekelezwa kuanzia usiku wa siku ya Ijumaa (kesho),” alisisitiza Rais huyo machachari.

Alisema zuio hilo pia litahusu biashara na usafirishaji wa mizigo kutoka Ulaya kuingia kuingia Marekani.

Kutokana na hofu hiyo, Rais Trump alitangaza kutoa mkopo wa mabilioni ya dola kwa wafanyabiashara wadogo.

Trump pia aliwataka wabunge wa Bunge la Congress kupitisha nafuu ya kodi ili kukabiliana na athari za mlipuko wa corona kiuchumi.

Rais huyo aliutupia lawama Umoja wa Ulaya (EU) kwamba umeshindwa kuchukua hatua za tahadhari kama hizo ili kutokomeza ugonjwa huo.

Awali Jimbo la Washington lilipiga marufuku mikusanyiko katika eneo hilo ambako ndiyo limeathirika zaidi na virusi hivyo. Kati ya watu 38 waliofariki dunia 24 wametokea katika jimbo hilo.

Katika hatua nyingine Serikali ya Italia imetangaza kufunga maduka yote isipokuwa yanayouza vyakula na dawa za binadamu.