Uamuzi wa Iraq kuyatimua majeshi ya nje wamwibua Trump

Muktasari:

  • Asema ataishambulia na kuiwekea vikwazo ambayo haijawahi kushuhudia

Washington. Siku moja baada ya wabunge wa Iraq kupitisha azimio la kutaka vikosi vyote vya kigeni kuondoka nchini humo, Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Iraq na kuweka vikwazo ambavyo nchi hiyo haijawahi kuona.

"Tumewekeza kiasi kikubwa sana cha fedha katika jeshi la anga huko. Kujenga msingi wake imetugharimu mabilioni ya dola. Hatutaondoka, labda kama watatulipa gharama tuliyotumia," Trump aliwaambia waandishi wa habari.

Hayo yamejiri baada ya Marekani kumuua kiongozi wa juu wa jeshi la Iran, Jenerali Qasem Soleimani katika shambulio la anga lililofanywa kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad, wiki iliyopita.

Soleimani ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 62, alikuwa akiongoza operesheni za vita katika nchi za mashariki ya kati na alikuwa anatambuliwa na Wamarekani kama gaidi.

Mwili wa jenerali huyo umerejeshwa katika nchi yake Iran, eneo ambalo maelfu waombolezaji wamekusanyika barabarani katika mitaa ya Tehran.

Kiongozi mpya wa kikosi cha jeshi la Iran la Quds - ambacho Soleimani aliongoza, naye ameapa kuwaondoa Wamarekani katika mataifa ya mashariki ya kati.

"Tumeahidi kuendelea kuwa mashahidi wa Soleimani kwa kufuata mwongozo wake na kile ambacho tunaweza kukifidia dhidi ya kifo chake ni kuwaondoa Wamarekani katika ukanda wetu," amesema Esmail Qaani.

Jana Jumapili Bunge la Iraq lilitoa wito kwa wanajeshi wote wa kigeni wanaotumia ardhi ya nchi hiyo, maeneo ya anga au maji kwa sababu zozote kuondoka haraka. Marekani ina wanajeshi 5,000 Iraq, kama washauri.

Akijibu uamuzi huo, Trump akiwa katika ndege ya rais, alisema kama Iraq inataka majeshi ya Marekani yaondoke nchini mwake kwa nguvu, "tutalipiza kwa kufanya mashambulizi ambayo hayajawahi kutokea kabla. Na kufanya vikwazo ambavyo Iran imeviweka kuwa vya kawaida sana."

Azimio sawa na la wabunge wa Irai kuwa majeshi yote ya kigeni yaondoke nchini humo, pia lilipitishwa na Bunge la Waislamu wa Shia ambao wako karibu na Iran.

Iran vilevile imetangaza kuwa haitazingatia tena vizuizi vilivyowekwa katika mkataba wa nyuklia kimataifa ulioanza mwaka 2015, ambao ulikuwa unawapa fursa wakaguzi wa kimataifa kuweka kikomo cha matumizi ya nyukia kwa makubaliano ya kuondoa vizuizi vya kiuchumi.