Uamuzi wa Prince Harry, mkewe kuachana na majukumu ya familia ya kifalme washtua

London. Mwanamfalme wa Uingereza, Harry na mkewe Meghan wametangaza kuachana na majukumu yao katika familia ya kifalme.

Kufuatia hatua hiyo, familia ya kifalme imeeleza kusikitishwa na maamuzi, ikisema ni kama ndoto huku ikihoji itakuwaje kuhusu suala la ulinzi wao.

Wanandoa hao wamesema sasa wanapanga kutumia muda wao mwingi Amerika ya Kaskazini na kujitegemea kifedha.

Taarifa iliyotolewa jana na Jumba la Kifalme Buckingham, imeeleza kuwa Prince Harry na Meghan wataendelea kumuunga mkono kikamilifu Malkia Elizabeth.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya makao makuu ya Malkia Elizabeth, mazungumzo yanaendelea kati ya Prince Harry na mkewe kuhusu mipango hiyo.

Familia ya  Kifalme imesema inaelewa kuhusu nia yao, lakini masuala hayo kwa sasa ni magumu na itachukua muda kuyafanyia kazi.

Hata hivyo, familia hiyo imesema haikuhusishwa na wala haikuwa na taarifa zozote za awali kuhusu maamuzi ya wanandoa hao.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), limebainisha kuwa si Malkia wala mwana mfalme William au waandamizi wengine katika falme walijulishwa kuhusu hatua hiyo na kwamba uongozi wa juu wa ufalme umepata pigo.

Kasri ya kifalme imesema suala hilo ni gumu sana na imelipokea kwa mshtuko mkubwa.

Katika maelezo yao, Prince Harry na Meghan walisema walifikiria uamuzi huo kwa muda mrefu na kufanya maamuzi hayo miezi mingi iliyopita.

Wanandoa hao wamepanga kugawa muda wao kwa nusu kuishi Marekani na nusu Uingereza, kuendelea kumtumikia malkia na kujihusisha na shughuli za kifalme.

"Maamuzi hayo yataturahisishia kumlea mtoto wetu katika makuzi ya utamaduni wa kifalme, na kuipa fursa familia kuangalia hatua inayofuata," walisema wapenzi hao.

Msemaji wa zamani wa malkia Dickie Arbiter alisema kuwa hafahamu ni namna gani wataweza kugeuza mipango yao.

"Hii ni kama ndoto. Kuna suala la usalama; nani atatoa ulinzi kwao?

"Je, ni nchi gani itawapa ulinzi wa kifalme? Je, ni Canada au? Na nani atagharamia?"

Oktoba mwaka jana Prince Harry na mkewe walilalamika kuingiliwa maisha yao kwa kufuatwa na vyombo vya habari kwa kivuli cha kutoka katika familia ya falme.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Prince Harry na mkewe wametoa utetezi wao kuhusu tangazo lao kwamba, wameifikia hatua hiyo baada ya kuwa na majadiliano ya ndani ya nyumba yao wao wawili kwa miezi kadhaa.

Hata hivyo, maamuzi yao yamepingwa kwa kudaiwa kuwa walistahili kupewa idhini ya jambo hilo na kutoa taarifa kabla.

Malengo yao mengine ya kujiondoa katika shughuli za moja kwa moja za kifalme ni kutaka kufanya kazi za kawaida katika kuendesha maisha yao ya kila siku badala ya kutegemea mapato yatokanayo na nafasi zao za kifalme.

Ingawaje wamesisitiza kwamba bado wataendelea kumuunga mkono Malkia na ufalme kwa ujumla.

Katika maelezo yake kupitia ukurasa wa instagram mwana mfalme Harry ameomba waruhusiwe kama kutekeleza walivyoamua, yeye na mkewe.