Uganda yasitisha hukumu ya kifo

Muktasari:

Kwa sasa Uganda inatekeleza hukumu ya adhabu ya kifo kwa uhalifu wa makosa makubwa.

Kampala, Uganda. Bunge la Uganda limefanya mabadiliko ya   sheria nne ikiwamo hukumu ya adhabu ya kifo.

Wabunge hao wamepitisha marekebisho hayo yanayopinga adhabu ya kifo leo Jumatano Agosti 21 katika mkutano wa Bunge hilo unaoendelea jijini Kampala.

Iwapo Rais Yoweri Museveni atatia saini marekebisho hayo yatasitisha hukumu ya kifo kwa uhalifu mkubwa zaidi.

Aidha, Bunge hilo pia limefanya mabadiliko katika sheria nyingine nne ikiwamo Sheria ya Kupambana na ugaidi.

Mabadiliko hayo yanaungwa mkono na wadau wa sheria nchini humo na kusema kuwa ni hatua kubwa katika kutetea haki binadamu.

Mara kwa mara wadau wa sheria nchini humo ikiwamo mahakama wamekuwa wakipigia kelele adhabu hiyo kwa madai kuwa inakiuka haki za binadamu.

Kumekuwa na kampeni mbalimbali za kutokomeza hukumu hiyo ambako mwaka 2009 mwanaharakati Susan Kigula alifungua kesi kupinga adhabu hiyo akisema kuwa inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi.

Mpaka sasa Uganda inawafungwa 133 ambao wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa ambao wamekaa kwa zaidi ya miaka 20 tangu wahukumiwe.