Uhuru, Raila wakutana faragha ufukweni Kisumu

Sunday June 16 2019

 

Nairobi. Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga juzi walifanya mazungumzo ya siri katika Klabu ya Yacht mjini Kisumu.

Viongozi hao waliwasili katika klabu hiyo iliyoko katika mtaa wa Milimani, ufukweni mwa Ziwa Victoria kwa msafara wa magari 12 pekee ambapo walipata chakula cha jioni huku wakifanya mazungumzo kwa saa moja.

Rais Kenyatta na Odinga walikuwa wametoka kuhudhuria mazishi ya mama ya Gavana wa Kisumu, Anyang Nyong’o katika Kijiji cha Ratta, jimbo la Seme.

Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na viongozi wengi,  yalikamilika saa 11:00 jioni kabla ya viongozi hao kupanda helkopta tofauti hadi uwanja wa ndege wa Kisumu.

Walipotua, walipanda katika gari moja na kuondoka wakizungumza, limeripoti Gazeti la Taifa Leo la  Kenya.

Magari kwenye msafara wa wawili hao hayakuwa yale wanayotumia katika shughuli rasmi kwani hayakuwa na ving’ora, bendera wala pikipiki za polisi kama ilivyo kawaida kwa msafara wa Rais.

Advertisement

Hali hiyo ilifanya wananchi kutotambua kwamba magari yaliyowabeba Rais Kenyatta na Odinga yalikuwa kwenye msafara.

Kabla ya kuelelea klabu hiyo, wawili hao walifanya ziara ya ghafla katika Chuo cha Mafunzo kuhusu Viumbe vya Majini (Marine Training Institute) kilichoko karibu na bandari ya Kisumu ambako walikagua shughuli za ujenzi zinazoendelea hapo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya gazeti hilo, mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na mtu mwingine ambaye hakutambuliwa japo alihisiwa kuwa mkuu wa utumishi wa umma, Joseph Kinyua.

Duru zilisema walishiriki mlo wa ugali wa rangi ya kahawia, samaki aina ya sato na mboga za kienyeji.

“Vilevile, waliagiza chupa kadha za bia na juisi huku wakipiga gumzo kwa muda wa takriban saa moja hivi,” akasema mhudumu mmoja katika klabu hiyo.

Ni katika klabu hiyo ambako viongozi hao walitembelea Januari 19 baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Hazina ya Ustawishaji wa Vijana, Bruce Odhiambo katika eneo la Muhoroni.

Wakati huo pia, Rais Kenyatta aliwashangaza walinzi wake na maofisa wa itifaki alipobadili mpango wa kusafiri uliopangwa na kuamua kujivinjari Kisumu akisafiri kwa magari ya kawaida.

Ijumaa, Rais alipowasili Yatch Club kwa mara ya pili akiandamana na Odinga na wageni wake wachache, wahudumu walichangamka huku viongozi hao wakielekea moja kwa moja katika chumba maalumu karibu na Ziwa Victoria.

“Kama kawaida yake, Rais aliwasalimia wateja na wahudumu kwa kuwapungia mikono kabla ya kuketi katika chumba hicho kilichokuwa na viti vinne,” mhudumu mmoja, ambaye aliomba asitajwe alisema.

Rais Kenyatta alisikika akifurahia upepo wa ziwa.

“Ziwa linafurahisha kwani gugumaji limepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na awali tulipokuwa hapa,” alisikika akisema.

Uwepo wa Dk Matiang’i katika mkutano huo wa Rais Kenyatta na Odinga unatokana na cheo alichotunukiwa cha mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya kushirikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali Kuu.

Vilevile, Waziri Matiang’i amekuwa haelewani na wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto wanayemchukulia kama anatumiwa kuzima ndoto zake kuingia Ikulu 2022.

Maafisa wengine wachache walioandamana na Rais Kenyatta na Odinga waliketi mahala tofauti kwa chakula cha jioni na vinywaji.

Mbunge wa Kisumu ambaye inadaiwa ndiye aliandaa mipango ya mkutano huo pia alionekana katika kilabu hiyo.

Lakini mawaziri wengine walioandamana na Rais mazishini, kama vile George Magoha (Elimu), Eugene Wamalwa (Ugatuzi), Sicily Kariuki (Afya) na Raphael Tuju hawakuwapo katika klabu hiyo.

Shughuli katika klabu hiyo maalum ziliendelea kama kawaida licha ya uwepo wa viongozi hao.

Majira ya saa moja na nusu usiku, viongozi hao wawili waliondoka kama walivyowasili na kuelekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu ambapo Rais Kenyatta alipanda helkopta ya kijeshi kurejea Nairobi.

Rais na ujumbe wake walipoondoka Yacht Club, maofisa wa Ikulu waliwazawadia wahudumu kwa hela chache “ kwa kazi nzuri”.

Advertisement