Uingereza kuchapisha ripoti kuhusu Urusi baada ya uchaguzi

Muktasari:

Wapinzani wanaituhumu Serikali kupitia kamati ya Bunge ya ujasusi na usalama kwa kukalia ripoti hiyo kwa kuwa inaweza kufichua mambo ya aibu dhidi ya Waziri Mkuu, Boris Johnson pamoja na chama chake.

London, Uingereza. Serikali ya Uingereza imesema kuwa itachapisha ripoti ya Bunge inayochunguza madai ya Urusi kuingilia siasa za nchi hiyo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mapema.

Kwa sasa nchi hiyo iko katika kampeni za uchaguzi wa mapema unaotarajiwa kufanyika Dasemba 12.

Waziri wa Usalama wa Uingereza, Brandon Lewis amekiambia kituo cha Televisheni cha Sky News kwamba ripoti hiyo huenda isichapishwe katika kipindi hiki tete cha kuelekea uchaguzi.

Wapinzani wanaituhumu Serikali kupitia kamati ya Bunge ya ujasusi na usalama kwa kuikalia ripoti hiyo ambayo imeshapitishwa na idara za usalama kwa kuwa inaweza kufichua mambo ya aibu dhidi ya Waziri Mkuu, Boris Johnson pamoja na chama chake.

Lakini Lewis amesema wanataka kuhakikisha wanachukua tahadhari hususan katika masuala yanayohusiana na usalama wa Taifa na kusisitiza kuwa ripoti hiyo itachapishwa baada ya uchaguzi.